HABARI KWA WAKATI KUTOKA HAPA

Tunakuhakikishia kupata habari zote zilizo muhimu kutoka ulimwenguni kote kwa wakati, unaweza kusubscribe mtandao wetu na ukawa unapokea habari zote katika email yako punde tu tuchapishapo machapisho yetu. Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

HABARI ZA MICHEZO

Sasa Fichuo tunakuhakikishia kupata taarifa zote za kimichezo kutoka viwanja mbalimbali duniani, lengo ni kuhakikisha hupitwi na lolote katika ulimwengu wa michezo.Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

TAARIFA ZA BURUDANI NA HABARI ZA WASANII

Unapenda masuala ya burudani? Ni jukumu letu kuhakikisha unazipata info zote za burudani na wasanii wanaokupa burudani, unapata video mpya, movie pamoja na muziki. Kaa karibu nasi.

KURASA ZA MAGAZETI KILA SIKU

Tunakupatia kila ambacho kinaandikwa katika magazeti ya Tanzania na nje ya Tanzania, usitie shaka ukishindwa kununua gazeti uipendalo, sogea karibu nasi na upate kila unachokihitaji.

MAHUSIANO

Fahamu mambo mengi katika ulimwengu wa mapenzi kwa kupitia dondoo, simulizi na visa mbalimbali kupitia Fichuo Online, Jiunge na mitandao yetu ya Facebook na Twitter kutupata kirahisi.

Alhamisi, Aprili 27, 2017

FAROE, KISIWA CHENYE UHABA WA WANAWAKE

Kuna upungufu wa wanawake katika kisiwa cha Faroe. Hivyobasi wanaume katika kisiwa hicho wanatafuta wanawake kutoka maeneo mengine kama vile mataifa ya Thailand na Ufilipino.
Lakini je ni changamoto gani zinazowakumba wanawake wanaoelekea katika kisiwa hicho.
Wakati Athaya Slaetalid alipoelekea katika kisiwa hicho ambapo kipindi cha majira ya baradi huchukua muda wa miezi sita alikuwa akikaa karibu na kikanza ama heater kwa jina la Kiingereza kwa siku nzima.
''Watu walikuwa wakiniambie niende nje kwa sababu kuna jua lakini nilisema'': ''Hapana niwacheni, nahisi baridi sana''.
Kuhamia katika kisiwa hicho miezi sita iliopita ilikuwa vigumu kwa Bi Athaya aliyekiri.
Alikutana na mumewe Jan alipokuwa akifanya kazi na rafikiye mmoja wa kisiwa hicho ambaye alikuwa ameanza biashara nchini Thailand.
Jan alijua mapema kwamba kumpeleka mkewe katika utamaduni huo, hali ya hewa itakuwa changamoto kubwa.
"Nilikuwa na wasiwasi kwa sababu kila kitu alichokiwacha nchini Thailand kilikuwa tofauti na kile alichokuja kuona katika kisiwa cha Faroe'', alisema.
''Lakini kwa sababu namjua Athaya nilijua ataingiliana na hali ya hewa''.
Kufikia sasa kuna takriban wanawake 300 kutoka Thailand na Ufilipino wanaoishi katika kisiwa cha Faroe.
Haionekani kuwa idadi kubwa lakini kisiwa hicho chenye idadi ya watu 50,000 sasa wanawakilisha watu walio wachache katika visiwa hivyo 18 kati ya Norway na Iceland.
Katika miaka ya hivi karibuni visiwa vya Faroe vimepata upungugufu wa wa idadi ya watu huku vijana wakiondoka ili kutafuta elimu na huwa hawarudi.
Kulingana na waziri mkuu Axel Johannese, kisiwa hicho kina upungufu wa jinsia huku kukiwa na uchache wa takriban wanawake 2000 ikilinganishwa na wanaume.
Hatua hiyo imewafanya wanaume katika kisiwa hicho kutafuta wanawake katika maeneo mengine kwa mapenzi.
Wengi ijapokuwa sio wote wa wanawake hao wa bara Asia, walikutana na wanaume zao kupitia mtandaoni wengine kupitia mitandao ya kukutanisha wapendanao.
Wengine wamepatana kupitia mitandao ya wanandoa wa Asia na visiwa vya Faroe.
Kwa wale wanaowasili, utamaduni wa eneo hilo unaweza kuwaathiri.
Vikiwa ni miliki za Denmark, visiwa vya Faroe vina lugha yao na utamaduni wa kipekee hususan katika maswala ya chakula.

ODINGA KUPEPERUSHA BENDERA YA UPINZANI KENYA

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA) umemteua aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka 2017.
Bw Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili.
"Hii ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito," alisema Bw Odinga akihutubu baada ya kutangazwa kuwa mgombea.
Amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.
"Sisi tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu".
Alisema serikali yake itaangazia kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kurejesha gharama ya elimu na maisha chini.
Bw Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari,pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.
Kadhalika, ameahidi akishinda serikali yake itamaliza rushwa serikalini.
Makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.
"Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa," amesema.
Amesema mpango wao ni kuwa wadhifa wa kinara wa mawaziri na msaidizi wake, kama ilivyokuwa kwenye rasimu hiyo ya katiba.
Mgombea mwenza wa Bw Odinga atakuwa makamu wa rais wa zamani Bw Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement.

DARASA LA FACEBOOK CHUO KIKUU

Kuandika ujumbe na kupakia picha na video limekuwa jambo la kawaida kwa karibu watu 1.8 bilioni wanaotumia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Ingawa ujumbe wako wa siasa au salama za heri, pongezi au rambirambi unaweza kupendwa na wenzako, si wengi wanaoweka kuchukulia ujumbe huo kuwa fasihi au kazi ya sanaa.
Lakini sasa Chuo Kikuu cha Delhi (DU) kimechukua msimamo tofauti.
Kinataka kujumuisha kuandika ujumbe wa Facebook kuwa sehemu ya mtalaa wake wa somo la Kiingereza.
Wanafunzi watakuwa wakifunzwa pia jinsi ya kuandika blogu au barua kuu ya kujitambulisha wakati wa kuwasilisha maombi ya kazi.
DU ni miongoni mwa vyuo vikuu bora zaidi nchini India.
Miongoni mwa waliowahi kusomea katika chuo kikuu hicho ni waziri mkuu Narendra Modi na kiongozi wa Burma na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Aung San Suu Kyi.
Mambo hayo yamejumuishwa kwenye mswada wa mtalaa wa Kiingereza ambao unatathminiwa na maprofesa wa DU.
Prof Christel Devadawson, mkuu wa kitivo cha lugha ya Kiingereza aktika chuo kikuu hicho, aliambia BBC kwamba ujumbe kwenye Facebook utatumiwa kama sehemu ya Kozi ya Kuimarisha Ujuzi - ambayo ni sehemu ya somo inayotumiwa kuwapa wanafunzi maarifa na ujuzi wa kuwawezesha kufaa maeneo ya kazi.
Gazeti la Hindustan Times linasema nchini India, mitandao ya kijamii inaweza kumzolea umaarufu mkubwa mwandishi chipukizi au msanii na kumuwezesha kufikia watu wengi au hapa kupata matbaa ya kuchapisha kazi zake.

Jumatano, Aprili 19, 2017

UHAKIKI WA VIBALI VYA UKAAZI SASA KIELEKTRONIKI

Serikali imezindua mfumo wa Kielektroniki wa Uhakiki wa Vibali vya ukazi “e-verification” hapa nchini ili kuongeza tija na kudhibiti upotevu wa mapato.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo huo.
Akizungumzia mfumo huo Kamishna Jenerali Makakala amesema utasaidia Makampuni, Taasisi, Mashirika na watu binafsi kuhakiki vibali vya watumishi wao ili kuona kama ni halali ama si halali na idara hiyo itakuwa tayari kuwasaidia wale wote watakaokuwa na matatizo kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
“Idara inatoa siku 90 kwa watu wote kuhakiki vibali vyao vya ukazi ili kama wana matatizo wasaidiwe kupata ufumbuzi” Alisisitiza Dkt Makakala.
Akizungumzia lengo la mfumo huo Makalala amesema utasaidia kuimarisha udhibiti wa wageni wanaoishi hapa nchini na kuzuia mianya ya upotevu wa maduhuli ya Serikali na mfumo huo ni rahisi na unatoa fursa kwa wageni wote wenye vibali vya ukaazi kuhakikiki kumbukumbu za vibali vyao ili kujua kama vimetolewa na Idara hiyo.
Aidha,Idara ya Uhamiaji inawaomba wadau wa huduma zake kufika wao wenyewe katika Ofisi zao katika ngazi ya Wilaya, Mikoa na Makao Makuu kwani huduma za Uhamiaji hazina uwakala.
Mfumo huo wa uhakiki wa vibali vya ukaazi kwa kutumia njia ya kielektroniki “e-verification” unapatikana kupitia tovuti ya uhamiaji ya www.immigration.go.tz.

Jumatatu, Aprili 17, 2017

MOVIE YA FATE OF THE FURIOUS YAVUNJA REKODI YA DUNIA

Filamu ya Fate of the Furious imevunja rekodi ya dunia ya kuwa filamu iliyouzwa sana baada ya kuzinduliwa rasmi.
Filamu hiyo, ambayo ni ya nane katika mwendelezo wa filamu za Fast & Furious, ilipata mauzo ya jumla ya $532.5m (£424.7m) duniani wikendi ya Pasaka.
Hayo ndiyo mauzo ya juu zaidi duniani kwa filamu yoyote siku zake za kwanza baada ya kuzinduliwa rasmi.

Filamu hiyo imepita mauzo ya $529m (£421.8m) rekodi ya awali iliyowekwa na Star Wars: The Force Awakens.
Mauzo hayo ya filamu hiyo nchini Marekani hata hivyo yalikuwa chini ukilinganisha na mauzo ya filamu iliyotangulia.
Furious 7 ilipata mauzo ya $147.2m (£117.3m) nchini Marekani ilipozinduliwa 2015.
Lakini filamu ya sasa imezoa $100.2m (£80m) pekee.
Licha ya kushuka kwa mauzo yake Marekani, filamu hiyo bado ilichangia sehemu kubwa ya mauzo ya filamu Marekani, ambapo ilichangia karibu theluthi mbili.
Mshindani wake wa karibu alikuwa The Boss Baby, ambayo iliuza $15.5m na kuwa ya pili.
Filamu za Fast & Furious zilianza kuuzwa 2001.
Ufanisi wa filamu hii ya sasa ulichangiwa sana na China ambapo mauzo yake yalikuwa $190m (£151m) kwa siku hizo tatu.
Vin Diesel, ambaye ameigiza katika kila filamu ya Fast & Furious amesema anashukuru sana na amefurahishwa sana na ufanisi wa filamu hiyo.
Wengine walioigiza katika Fate of the Furious ni Charlize Theron, Tyrese Gibson na Ludacris.
Filamu nyingine za Furious zitatolewa mwaka 2019 na 2021.

ALIYEMCHEZA JAMES BOND AFARIKI DUNIA

Mwigizaji Clifton James, aliyeigiza kama Liwali JW Pepper kwenye filamu mbili za James Bond, amefariki dunia akiwa na miaka 96.
Alifariki karibu na mji wake aliokulia wa Gladstone, Oregon, siku ya Jumamosi kutokana na matatizo ya ugonjwa wa kisukari.
James alifahamika sana kutokana na uigizaji wake pamoja na Sir Roger Moore katika filamu za Bonds za Live and Let Die na The Man with the Golden Gun miaka ya sabini.
Binti yake Lynn amesema: ''Alikuwa mtu mpenda watu na mwenye uwazi sana. Alipendwa sana na kila mtu.''
Aliongeza: "Sidhani alikuwa na adui hata mmoja. Kwa kweli tulibarikiwa kuwa na yeye maishani."

ZIMBABWE SASA KULIPA MIFUGO SHULENI BADALA YA ADA

Serikali ya Zimbabwe imeruhusu wazazi kulipa ada kwa mifugo au kwa kufanya kazi ktk shule husika kama malipo.
Waziri wa Elimu ya Msingi na Sekondari, Dr. Lazarus Dokora amesema kwamba mamlaka za shule zinatakiwa kubadilika na kuacha kufukuza watoto kwa kuwa tu wazazi wao hawana pesa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dr. Sylvia Utete-Masango alifafanua kuwa mifugo itatumika kulipa kwa wazazi wa maeneo ya vijijini tu na mijini wazazi watalazimika kufanyakazi kama ujenzi kwenye shule husika endapo hawana pesa.
Zimbabwe inakabiliwa na uhaba wa pesa tangu mwaka jana baada ya Serikali kutishia kutaifisha makampuni yote ya kigeni nchini humo chini ya sheria ya kurudisha kila kitu kwa wazawa (Indigenisation and Empowerment Law).
Benki zililazimika kupunguza kiwango cha kutoa pesa hadi $40 kwa siku kwa kila mtu mmoja.

Jumamosi, Aprili 15, 2017

POLISI MBEYA YAKAMATA WAHAMIAJI HARAMU 66 KUTOKA ETHIOPIA

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:- 
Mnamo tarehe 14.04.2017 majira ya saa 15:00 Alasiri huko katika Kijiji cha Simambwe kilichopo Kata na Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini katika Barabara kuu ya Mbeya kuelekea Tukuyu Wilaya ya Rungwe, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 66 wote wanaume, umri kuanzia miaka 14 hadi 35 na wote raia wa nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wahamiaji hao walikamatwa baada ya Gari walilokuwa wakisafiria yenye namba za usajili T.913 AVM aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye PRINCE MATHEW (25) Mkazi wa Kijiji cha Kadia Mkoa wa Kilimanjaro kusimamishwa na askari wa usalama barabarani waliokuwa katika majukumu yao na kisha kufanya ukaguzi wa kawaida wa  gari hilo na ndipo waligundua kuwa gari hilo limebeba wahamiaji haramu.
Aidha baada ya kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu, dereva wa gari alihojiwa na kueleza kuwa aliwachukua watu hao kutoka eneo la Msata – Bagamoyo kwa ajili ya kuwapeleka Kasumulu Wilaya ya Kyela ili wavushwe kuelekea nchi jirani ya Malawi. 
Taratibu za kisheria zinafanyika ili wahamiaji hao wakabidhiwe Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria. Wakati huo huo, dereva wa gari PRINCE MATHEW anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu. Mahojiano zaidi yanaendelea ili kubaini na kuwakamata wahusika wote ikiwa ni pamoja na mtandao mzima wa wasafirishaji wa wahamiaji haramu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahamiaji haramu na wahalifu kwa ujumla katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za siri zitakazofanikisha kukamatwa. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kusherehekea kwa amani na utulivu sikukuu ya Pasaka ikiwa ni pamoja na kifuata sheria za nchi na kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa aina yoyote. Pia anawataka wazazi na walezi kuwa makini hasa kwa watoto wadogo pindi waendapo maeneo yenye mikusanyiko kama vile kanisani.

Alhamisi, Aprili 13, 2017

MUONEKANO MPYA WA RAIS MUGABE

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe kwa mara ya kwanza amepigwa picha akiwa amenyoa nyele zake wakati alipohudhuria mazishi ya mwanajeshi wa zamani.
Wengi wanaamini ni mara ya kwanza Mugabe kunyoa nywele zake na hata masharubu.
Picha zilizochapishwa katika mitandao ya kijamii zimevutia maoni kutoka kwa raia wa Zimbabwe
Baadhi wamesema kuwa mtindo alionyoa umechangia aonekane kijana.
Lakini hata hivyo wengine wanasema kuwa wameshangaa kuwa nia yake ni ipi.
Labda kubadilisha mtindo wa ni jambo limenza kuiwa na viongozi wa nchi. Rais wa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo Joseph Kabila pia naye alipigwa picha akiwa na mtindo mpya wa nyele nyingi kichwani alipohudhuria wabunge wiki iliyopita.

WATANZANIA WALIOSHIKILIWA KWA UJASUSI MALAWI WAACHILIWA

Watanzania wanane waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya ujasusi, nchini Malawi wameachiwa huru jana na sasa wapo njiani kurejea nchini Tanzania .
Hukumu ya kesi yao ilitolewa jana jioni tarehe 12 mwezi Aprili mwaka huu,Watanzania hao waliokuwa wanashikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani uliopo eneo liitwalo Kayerekera.
Serikali ya Tanzania ilikataa kwamba Watanzania hao walitumwa na serikali ili kufanya shughuli za kijasusi katika mgodi huo wa urani. Tanzania iliongeza kwamba watu hao walikuwa ni wafanyakazi wa Taasisi ya misaada ya Caritas iliyo chini ya Kanisa Katoliki Jimbo la Songea mkoani Ruvuma.
Wakili aliyekuwa anaisimamia kesi hiyo ,Flaviana Charles ameiambia BBC kuwa watu hao kwa sasa wako huru pamoja na kuwa wamepitia katika magumu mengi na ya kukatisha tamaa lakini kila kitu kilikuwa wazi na upande wa walalamikaji hawakuwa na ushaidi wa kutosha wa kuwafunga kwa kuwa watanzania hao waliingia nchini humo kihalali kuanzia mpakani na walikuwa na mualiko na wakati wanawakamata walikuwa hawajafika mgodini bado maana walikamatwa wakiwa wanatoka hotelini hivyo hawakufika mgodini au kuhoji mtu yeyote hivyo shutuma zao zilikuwa zenye mashaka sana.
Je,kuna fidia ambayo wamelipwa baada ya kuwekwa kizuzini tangu mwezi desemba mwaka jana?
Wakili Flaviana amesema kuwa kuna ujanja ambao mahakama imeutumia ili kukwepa fidia kwa kudai kuwa ambayo wameshatumikia kifungo kwa kipindi hicho chote watuhumiwa hao walipokuwa kizuizini hivyo kwa sasa wako huru.
BBC imezungumza pia na baadhi ya watu hao waliokuwa wanatuhumiwa,,wanasema wana furaha sana maana walikuwa wameenda Malawi kwa matarajio ya kukaaa siku 3 lakini sasa wamejikuta wamekaa zaidi ya miezi mitatu,bila kujua kinachoendelea katika familia zao pamoja na shughuli zao za kila siku
wamesema walikuwa wakiteseka bila sababu ilhali nia yao kwenda Malawi ilikuwa njema kabisa .
Watanzania hao nane,wanashukuru sana serikali yao ya Tanzania haswa kwa balozi kufika kuwaona.

Jumatano, Aprili 12, 2017

ONTLAMETSE AFARIKI DUNIA

Afrika Kusini inaomboleza kifo cha Ontlametse Phalatse, msichana wa umri wa miaka 18 ambaye alikuwa anaishi na ugojwa unaojulikana kama Progeria, ambayo ni hali ya kimaumbile isiyo ya kawaida ambayo husababisha mtu kuzeeka kwa haraka.
Mwezi uliopita Ontlametse alisherehekea siku ya kuzaliwa na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Seriklia ya Afrika kuisni imeongoza taifa kutuma rambi rambi kufuatia kifo hicho.
Alifariki hiyo jana katika hospitali ya Dr George Mukhari Academic iliyo nje ya mji wa Pretora.
Phalatse alikuwa mmoja wa wasichana wawili waliokuwa na hali hiyo nchini Afrika Kusini.
Alijiita "mama wa kwanza" , baada ya kuwa mtoto wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini, kupatikana akiwa na ugonjwa wa Progeria.
Alitajwa kuwa mtoto wa kuwapa watu motisha na mtot wa miujiza baada ya kuishi kuliko matarajio walioyokuwa nayo madaktari waliosema kuwa angefariki miaka minne iliyopita.
Rais Zuma ametuma rambi rambi zake kwa familia ya msichana huyo.

MWANAMKE AMBAKA DEREVA TAXI

Mwanamke mmoja katika jimbo la Ohio nchini Marekani ameshtakiwa kwa kum'baka dereva mmoja wa teksi kwa kutumia kisu kabla ya yeye na mwanamume mwengine kumuibia kulingana na maafisa wa polisi.
Brittany Carter mwenye umri wa miaka 23, anadaiwa kufanya tendo la ngono na dereva huyo mwenye umri wa miaka 29 huku Corey Jackson mwenye umri wa miaka 20 akimshikia kisu shingoni.
Maafisa wa polisi wanasema kuwa wawili hao waliiba dola 32 kutoka kwa mwathiriwa kabla ya kutoroka katika eneo la mkasa katika mji wa Findlay.
Hatujui ni kwa nini alifanya hivyo,luteni wa polisi Robert Ting alisema.Pengine ilikuwa hali ya kumpumbaza kwa sababu pia walimuibia pesa .
Mtuhumiwa Brittany Carter
Unyanyasaji huo ulitokea baada ya bi Carter kumuita dereva wa teksi hiyo ya kampuni ya Trinity Express Cab mapema mnamo tarehe 28 mwezi Januari, kulingana na maafisa wa polisi.
Alikamatwa baada ya dereva kuripoti kisa hicho .
Bi Carter anakabiliwa na shtaka la ubakaji pamoja na lile la uhalifu katika mahakama ya kaunti ya Hancock.
Alishtakiwa mara mbili kwa makosa ya dawa za kulevya mwaka 2016 na anadaiwa kumiliki dawa ya kulevya aina ya heroine.
Bi Jackson hajakamatwa huku agizo la kukamtwa likitolewa kulingana na polisi.
Anashtakiwa kwa kuchochea wizi na njama ya kutaka kufanya ubakaji.

Alhamisi, Aprili 06, 2017

NAPE NNAUYE KUMWAGA UKWELI WOTE JUMAMOSI


Aliyekuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kabla ya  Dkt. Harrison Mwakyembe kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo na rais wa nchi, Nape Mosses Nnauye ambaye ni mbunge wa jimbo la Mtama amearifu kuwa siku ya jumamosi atakuwa jimboni kwake kuzungumza na wananchi kuhusu ukweli wa kila kilichotokea.
Nape ametoa taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa Twitter mapema leo.
Shukrani kwa wote mlioniunga mkono katika kusimamia haki. Narudi Mtama kuwaeleza wapiga kura wangu UKWELI WOTE. Ni Jmosi hii tar 8/4/17.

LILICHOZUNGUMZA SHIRIKISHO LA SOKA ULAYA (UEFA) KUHUSU MBWANA SAMATTA

Shirikisho la Soka Barani Ulaya(UEFA) katika ukurasa wao wa mtandao wa Twitter wametweet picha ya nyota wa soka kutoka Tanzania, Mbwana Ally Samatta na kumtaja kuwa ni mchezaji wa kuangaliwa.
Mshambuliaji huyo hatari amefunga magoli sita katika michezo mitano ya mwisho aliyoichezea Klabu yake ya KRC Genk.

KIONGOZI WA FREEMASON AFRIKA MASHARIKI AFARIKI DUNIA

Aliyekuwa mfanyabiahsra maarufu wa Tanzania na kiongozi wa ‘Freemason’ Afrika Mashariki, Jayantilal Keshavji “Andy” Chande amefariki dunia leo Nairobi nchini Kenya.
Jayantilal Keshavji “Andy” Chande alizaliwa May 7, 1928 Mombasa Kenya, na wakati wa utoto wake aliishi Bukene mkoani Tabora ambako ndiko alikopata elimu yake ya msingi.
Elimu yake ya sekondari aliipata katika Shule ya St. Peter’s School iliyoko Panchgani, walaya ya Satara, Jimbo la Maharashtra nchini India. Baada ya kufanya vizuri katika mitihani yake ndipo alipopata jina jipya la ‘Andy’ ambalo ndilo alikuwa akilitumia mpaka mauti yalipomkuta.
Baada ya kumaliza masomo yake, alirudi nchini Tanzania na kuendelea kumsaidia baba yake katika shughuli za kibiashara.
Mnamo mwaka 1967 wakati azimio la Arusha lilipopitisha sera ya utaifishaji, mali nyingi zilitaifishwa na kuwa za serikali. Ujuzi aliokuwa nao Andy ulimfanya Mwl. Nyerere amteue kuwa Meneja Mkuu wa Shirika la Taifa la kuhifadhi nafaka (National Milling Corporation)
Mpaka kufikia mwaka 2015 alikwa na utajiri wa dola za kimarekani milioni 892 sawa na TZS trilioni 1.9.
Wakati wa uhai wake amewahi kupokea tuzo mbalimbali ikiwemo ya (Knight Commander of the Most Excellent Order of the British Empire) KBE mwaka 2003 ambayo ilikuwa ni kwa mara ya kwanza kupewa raia wa Tanzania.

Jumatano, Aprili 05, 2017

CHELSEA YAONESHA UBABE MBELE YA PEP GUARDIOLA

Vinara wa ligi kuu ya England, Chelsea wamendeleza wimbi la ushindi katika ligi hiyo baada ya kuichapa Manchester City kwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Stanford Bridge.
Chelsea walipata mabao yao yote mawili kupitia winga wao mahiri Eden Hazard, huku bao la Man City likifungwa na Sergio Aguero.
Arsenal wakicheza katika uwanja wao wa Emirate waliwachapa West Ham kwa mabao 3-0 na hivyo Arsenal kurejea katika nafasi ya tano.
Liverpool wakashindwa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani baada ya kukubalia sare ya mabao ya 2-2 na AFC Bournemouth, Hull City wao wakashinda kwa mabao 4-2 dhidi ya Middlesbrough.
Tottenham Hotspur wakicheza ugenini katika dimba la Libery waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Swansea City, Southampton wakashinda kwa 3 - 1 dhidi ya Crystal Palace.

Jumanne, Aprili 04, 2017

WEMA SEPETU KUSHINE KATIKA JARIDA LA KENYA 'TRUE LOVE'

Safari yake ilianza rasmi mwaka 2006 alipojitwalia taji la Miss Tanzania, akaendelea kujenga jina lake taratibu alipoingizwa rasmi katika ulimwengu wa filamu Tanzania na marehemu Steven Kanumba, akaendelea kukaa katika kilele cha ustaa kwa miaka 10 kutokana na kufanya mambo mengi yaliyovutia watanzania wengi kupitia kampuni yake ya Endless Fame, na hata kuingia katika siasa ndani ya CCM. 
Sasa anaendelea kukaa kwenye vichwa vya watu baada ya kuingia katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kama haitoshi hivi karibuni tutamuona katika jarida kubwa kutoka nchini Kenya la TRUE LOVE! Anaitwa Wema Abraham Sepetu.
Katika ukurasa maaumu wa instagram wa jarida hilo waliyaandika haya:
This month Tanzania’s Sweetheart, the gorgeous @wemasepetu graces our cover. She opens up about Money, Men, Love and Loss. Be sure to grab a copy to see what she has been up to and also read about Easter plans and gateways. Happy new month’- True Love Magazine East Africa

ALICHOZUNGUMZA MTOTO BRADLEY LOWREY KUHUSU KIFO CHAKE NA JERMAINE DEFOE

Mtoto Bradley Lowrey ambaye anaumwa ugonjwa wa kansa unaojulikana kama Neuroblastoma ambaye madaktari bingwa wa ugonjwa wa kansa duniani walimtabiria kuwa hakuwa na siku nyingi za kusihi, amenukuliwa akisema kuwa kila anapojisikia kuumwa sana na kudhani kuwa anakaribia kufa kama alivyoambiwa na madaktari, anakumbuka maneno ya rafiki yake mkubwa Jermaine Defoe akisema:
“Bradley, huwezi kufa kwa ajili ya kuumwa, na endapo utakufa itakuwa ni kwa amri ya Mungu na utakuwa katika mikono salama."

BAADA YA KITILA MKUMBO KUTEULIWA NA RAIS, ZITTO KABWE AMETOA MSIMAMO WAKE NA CHAMA

Zitto Kabwe, kiongozi wa ACT-Wazalendo amesema walifanya mashauriano kama chama ikiwemo Kitila Mkumbo, chama kimepokea uteuzi wa Kitila kuwa katibu mkuu. Uteuzi unaonyesha upinzani kuna watu wenye uwezo, weledi na uzalendo wa kuweza kutumika katika utumishi wa Umma.
Kitila ni mtumishi wa umma kwa sababu ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Dar es Salaam kwa hio nafasi aliyopata ni kupanda cheo tu ndani ya utumishi wa umma, ni sawa kama angeteuliwa kuwa Vice Chancellor wa chuo kikuu.Kwa nafasi ya katibu mkuu, Ndugu Kitila hawezi kuendelea kuwa mshauri wa chama, nafasi ambayo inamfanya ahudhurie vikao vyote vya chama kuanzia ngazi ya chini mpaka kamati kuu na kamati ya uongozi.Prof. Kitila ameandika barua ya kujiuzulu ushauri wa chama, nimeipokea barua yake na nimemkubalia kujiuzulu kwake kuanzia Leo. Chama kinamshukuru sana mheshimiwa Kitila kwa wakati wote alichokitumikia chama toka tulipoanza chama hiki alipokuwa mshauri wa chama.Kaulimbiu yote siku zote ni taifa kwanza, leo na kesho hivyo tunamtakia kila laheri ndugu Kitila katika nafasi hii mpya, wizara ni kubwa na muhimu katika nchi yetu.Kwa hatua hii tumeona Rais ameamua kuunganisha nchi yetu kwa kufanya kazi na watu wote bila kuwabagua kwa itikadi zao za vyama. Watanzania ni wamoja na kauli za kuwagawa zinawaumiza zaidi. Tunaamini katika uteuzi huu, Rais ana nia njema na sisi tumempa baraka zote mwanachama wetu mwanzilishi wa chama kwenda kufanya kazi kwenye nafasi ya juu zaidi ya utumishi wa umma.
Alisema Zitto Kabwe

'UNDERTAKER' ASTAAFU MIELEKA

Mashabiki wa mchezo wa mieleka WWE walitokwa na machozi mwishoni mwa wiki wakati mcheza mieleka mashuhuri The Undertaker alipotangaza kustaafu kucheza mchezo huo baada ya miaka 25.
Katika mchezo wake wa mwisho Undertaker alipigwa na Roman Reigns na kuondoka ulingoni akiwa na rekodi ya kushindi michezo 23 na kupoteza miwili Wrestlemania.
Wakati akitoka ulingoni Undertaker alifanya kitu ambacho hajawahi kufunga hadharani kwa kwenda kumkumbatia mkewe Michelle McCool baada ya mechi dhidi ya Roman Reigns.
Akithibisha kustaafu kwake mchezo huo Undertaker aliacha katikati ya ukumbi koti lake, kofia na glovisi zake na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake.

BEI ZA PETROLI, DIZELI NA MAFUTA YA TAA ZAPAA

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zitakazoaanza kutumika kuanzia kesho. 
Akitangaza bei hizo leo (Jumanne)Meneja wa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo aliwaambia wanahabari kuwa petroli imeshuka Sh 3 itauzwa Sh 2057 kutoka 2060, dizeli imepanda kwa Sh 12, kutoka Sh 1913 hadi 1925 na mafuta ya taa ni Sh 1958 kutoka 1952.
"Mabadiliko haya bei yametokana na bei za mafuta katika soko la dunia kubadilika sanjari na mfuko wa bei na gharama za usafirishaji ikilinganishwa na mwezi uliopita,"amesema Kaguo.

MBARAKA YUSUPH WA KAGERA FC MCHEZAJ BORA VPL MWEZI MACHI

Mchezaji wa timu ya Kagera Sugar FC, Mbaraka Yusuph Abeid amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom wa mwezi Machi kwa msimu wa 2016/2017.
Mbaraka aliwashinda wachezaji Abubakar Salum wa Azam FC na Kenny Ally wa Mbeya City kutokana na kuonyesha kiwango cha hali ya juu, hivyo kuisadia timu yake kupata matokeo mazuri.
Katika mwezi huo ilichezwa raundi moja tu na Mbaraka ambaye alicheza kwa dakika zote 90 aliisaidia timu yake kukusanya pointi zote tatu zilizoifanya timu yake kubaki katika nafasi ya nne (4) katika msimamo wa ligi kwa mwezi huo.
Katika mchezo huo mmoja, Mshambuliaji huyo alifunga goli moja, na alionyesha nidhamu ya hali ya juu, hivyo kutopata onyo lolote la kadi.
Kwa kushinda tuzo hiyo, Mbaraka atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom Tanzania PLC.

WAFANYABIASHARA WATAWANYWA KWA SILAHA ZA MOTO MWENGE

Jeshi la Polisi limetumia silaha za moto kuwatawanya wafanyabiashara katika eneo la Mwenge, wilayani Kinondoni leo.
Taharuki iliwakumba wakazi wa eneo hilo mara baada ya polisi hao kuanza kuwatanya wafanyabiashara hao waliofunga barabara wakishinikiza magari yaruhusiwe kupaki katika eneo hilo.
Inaelezwa kuwa polisi wamezuia watu kupaki magari katika eneo hilo hali iliyosababisha wafanyabiashara hao kutofungua biashara zao leo. 
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wafanyabiashara na shuhuda wa tukio hilo, Musa Godwin alisema polisi walifika sokoni hapo saa12 asubuhi na kutawanya wafanyabiashara waliofunga barabara kuzuia polisi magari yasiegeshwe eneo hilo.
"Walifika hapa sokoni saa 12 asubuhi na baadhi ya watu walifunga njia ikasababisha polisi wapige risasi hewani, hadi sasa wanazunguka hapa kuzuia magari ambao ni wanunuaji wetu," alisema Godwin. 

Mwananchi.

BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UGANDA YAPOROMOKA

Katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania Bw. Ramadhani Mwinyi amesema, thamani ya biashara kati ya Tanzania na Uganda imeshuka tangu mwaka jana.
Amesema, mwaka jana thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia dola milioni 98 za kimarekani, na kwamba nchi hizo zinatakiwa kufanya juhudi kukabiliana na changamoto hiyo.
Pia amesema, sekta nyingi kutoka nchi hizo mbili zinatakiwa kutafuta chanzo cha kusababisha kushuka kwa biashara kati yao, hali isiyolingana na ushirikiano na uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili.

MHE. SALMA KIKWETE AAPISHWA DODOMA, KIKWETE ASHANGILIWA BUNGENI

Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania Job Ndugai leo amemuapisha mke wa rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, Salma Rashid Kikwete kuwa mbunge wa Bunge wa kuteuliwa.
Mh.Salma aliandamana na mumewe rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, ambaye uwepo wake ulisababisha kelele za shamra shamra kutoka kwa wabunge wakisema kwa sauti 'tumekumiss tumekumiss'.
Mkutano wa saba wa bunge la Tanzania umeanza kikao chake cha kwanza cha mkutano wa bajeti hii leo.
Mama Salma kama anavyotambulika na wengi nchini ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM, lakini pia anatajwa kuwa na ushawihi mkubwa sana wa kisiasa ndani ya chama chake.

RAIS MAGUFULI AMEMTEUA KITILA MKUMBO KUWA KATIBU MKUU WIZARA YA MAJI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli mapema leo amefanya mabadiliko ya Makatibu Wakuu kwa baadhi ya Wizara  ambapo katika mabadiliko hayo amemteua Prof. Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji.
Wateule wote wa Rais wataapishwa kesho tarehe 05 Aprili, 2017 saa 3:00 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Maelezo zaidi ya habari hii yako katika kielelezo hiki hapa chini

Jumatatu, Aprili 03, 2017

RATIBA YA BUNGE LINALOANZA LEO

Waziri wa Fedha na Uchumi Dkt Philip Mpango anatarajiwa kusoma Bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2017/18 siku ya Alhamisi, Juni 15 mwaka huu. 
 Tarehe hiyo ni kwa mujibu wa ratiba ya Mkutano wa Saba wa Bunge unaoanza leo Jumanne (Aprili 4) katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, mkutano ambao ni maalum kwa ajili ya bajeti. 
 Ratiba hiyo inaonesha shughuli ya kwanza kuwa ni uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki siku ya Jumanne, na Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu itasomwa siku ya Alhamisi, Aprili 6 na kujadiliwa kwa siku nne, ikifuatiwa na bajeti ya Rais (siku 4) na Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Siku 1) kabla ya bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba Aprili 25. Mbali na bajeti za wizara, mkutano huo pia utajadili na kupitisha miswada kadhaa ya sheria ukiwemo Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka, 2017

TRUMP KUFIKISHWA MAHAKAMANI??

Jaji mmoja wa Mahakama ya Shirikisho ya jimbo la Kentucky la nchini Marekani amemtuhumu Rais Donald Trump wa nchi hiyo kuwa alichochea machafuko wakati wa kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo kwa mujibu wa Press TV, David G. Hill, jaji wa mahakama moja ya shirikisho la Marekani huko Kentucky amesema kuwa, Donald Trump amekanusha madai yaliyotolewa dhidi yake ya kwamba alichochea machafuko wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2016.

Pamoja na hayo, jaji huyo ametoa hukumu inayoruhusu kufuatiliwa mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya Trump na timu yake ya kampeni. 
Jaji huyo wa Mahakama ya Shirikisho ya Marekani aidha amesema, kuna ushahidi wa kutosha wa kuthibitisha kwamba kulitokea machafuko wakati wa kampeni za uchaguzi za Donald Trump, na kusema kwamba rais huyo wa Marekani alisababisha machafuko hayo.
Mawakili wa Donald Trump wamefanya juhudi za kuzuia kesi za walalamikaji watatu ambao wanasema kuwa, mwezi Machi 2016 walishambuliwa kwa kupigwa na kutukanwa na wafuasi wa Trump wakati rais huyo wa Marekani alipokuwa anahutubia wafuasi wake katika jimbo la Kentucky. 
Wanawake wawili na mwanamme mmoja wamefungua kesi mahakamani dhidi ya Donald Trump wakilalamika kuwa, walishambuliwa na kutukanwa na wafuasi wa Trump kwa amri ya rais huyo wa Marekani.
Matamshi ya jaji huyo wa Mahakama ya Shirikisho ya Marekani ya kwamba Trump alichochea machafuko na kupigwa walalamikaji hao, linahesabiwa kuwa ni pigo jingine la kisheria kwa rais huyo mwenye chuki dhidi ya wageni, watu wasio Wazungu na pia dhidi ya Waislamu.

UMASIKINI KUONGEZEKA MAREKANI

Taasisi ya utafiti ya Gallup yenye makao yake makuu mjini Washington Marekani imetangaza habari ya kuongezeka idadi ya wananchi wa nchi hiyo walio na wasiwasi wa kupanda kiwango cha ukata hasa kati ya watu wa pato la chini na tabaka la watu masikini nchini humo.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi hiyo kuanzia tarehe mosi hadi tarehe tano mwezi uliopita wa Machi unaonesha kuwa, karibu asilimia 67 ya Wamarekani wenye kipato cha chini wana wasiwasi mkubwa wa kukumbwa na umaskini mkubwa zaidi na kupoteza makazi yao. Uchunguzi huo unaonesha kuweko ongezeko kubwa la Wamarekani wenye wasiwasi wa kukumbwa na matatizo hayo ikilinganishwa na miaka ya 2010 na 2011.
Uchunguzi wa huko nyuma wa maoni ulionesha kuwa asilimia 51 ya raia wa Marekani walikuwa na wasiwasi wa kuongezeka umaskini na kupoteza makazi yao.
Utafiti wa shirika la Gallup uliofanywa mwaka 2014 nchini Marekani ulionesha kuwa idadi ya Wamarekani waliokuwa na wasiwasi wa kupoteza makazi yao na kuongezeka umaskini wao haikupindukia asilimia 35 wakati huo.
Machafuko, vitendo vya utumiaji mabavu, uhalifu, jinai na ukosefu wa amani na usalama ni mambo mengine yanayozifanya nyoyo za wananchi wa Marekani kuwa na wasiwasi mkubwa hususan kati ya matabaka ya watu maskini na wenye kipato cha chini.
Matokeo ya uchunguzi wa hivi sasa wa taasisi ya Gallup unaonesha kuwa Wamarekani wa matabaka yote wana wasiwasi wa kupoteza makazi yao na kuongezeka umaskini na kwamba idadi yao imeongezeka sana hivi sasa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.

MWANAUME ALIYEAMUA KUATAMIA MAYAI YA KUKU

Msanii kutoka Ufaransa Abraham Poincheval anaendelea kutamia mayai ya kuku akiwa na matumaini kwamba mwishowe yataangua vifaranga.
Msanii huyo anatumia joto kutoka kwa mwili wake kutamia mayao hayo 10.
Poincheval ambaye hufanya uigizaji wa kuigiza mambo ya ucheshi lakini ya hatari tayari ameishi wiki mbili ndani ya dubu, miongoni mwa mambo mengine ya kushangaza.
Atakuwa katika chumba maalum ambacho anatamia mayai, ambapo watalii wanaweza kumtazama katka makumbusho ya Palais de Tokyo mjini Paris.
Anatarajia kutamia mayai hayo kwa siku 21 hadi 26.

MARUFUKU YA WANAUME MASIKINI KUOA WAKE WENGI NIGERIA

Spika wa bunge katika jimbo lililo kaskazini mwa Nigeria la Kano, amesema kwa umma utaombwa kutoa maoni yake kuhusu mswada wenye lengo la kuwazuia wanaume maskini kuoa zaidi ya mke mmoja.
Alhassan Rurum aliiambia BBC kuwa viongozi na wasomi wataombwa ushauri kuhusu ni tata t haswa atatambuliwa kuwa maskini.
Pendekezo hilo lenye utata lilitolewa na Muhammad Sanusi II, ambaye ni Emir wa Kano, kuhakisha kuwa wanaume wana familia ambazo wanaweza kuzitunza.

SERENGETI BOYS YAWASHANGAZA WAGHANA

Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imewashangaza vijana wa timu ya Taifa ya Ghana (U17) baada ya kuchomoa mabao mawili katika dakika za nyongeza na kupata sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Mchezo huo ni wa mwisho kwa Serengeti hapa nchini kwani Aprili 5 timu hiyo itaondoka kuelekea Morocco kwa ajili ya kambi ya mwezi mmoja kabla ya kwenda Gabon kwenye michuano ya Afrika kwa vijana itakayoanza mwezi ujao.
Sulley Ibrahim aliipatia Ghana bao la kuongoza dakika ya 21 kwa shuti kali ndani ya 18 lililomshinda mlinda mlango wa Serengeti Ramadhan Kabwili na kutinga wavuni.
Katika mchezo huo wachezaji wa Serengeti walikuwa wakicheza taratibu huku mipango yao ikishindwa kutimia mara kwa mara baada ya kuzidiwa ujanja na vijana wa Ghana.
Arko Mensah aliipatia bao la pili Ghana kwa mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya 18 alioupiga kiufundi na kutinga moja kwa moja wavuni.
Serengeti walisawazisha mabao hayo katika dakika za nyongeza kupitia kwa Assad Juma kwa mkwaju wa penalti kabla Muhsin Malima hajafunga bao la pili mwishoni kabisa mwa mchezo.

WALICHOKIZUNGUMZA NEY WA MITEGO NA MWAKYEMBE HIKI HAPA

Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, hatimaye amerejea kutoka Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma, ambapo alienda kuitikia wito wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison George Mwakyembe.
Hivi karibuni Nay alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuachia Wimbo wa Wapo uliokuwa na mashairi ya kuilenga serikali lakini baada ya siku chache Waziri Mwakyembe alitoa agizo la kuachiwa msanii huyo na wimbo huo kupigwa baada ya kusikilizwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli na kufurahishwa nao.

Baada ya Jeshi la Polisi kumuachia Nay, waziri alimuomba kufika Dodoma kukutana naye na kuzungumza mengi kuhusiana na sanaa. Over Ze Weekend limekuchambulia alichoambiwa;
“Nimeshaonana na Waziri Mwakyembe, kufuatia wito wake, ambapo nilifika hadi kwenye ofisi zake na tuliongea mambo mengi ikiwemo yeye kuniulizia kwa makini tungo yangu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa katika maongezi yetu alionekana akisifia sana kazi zangu.
“Kubwa zaidi aliloniambia yaani ikiwa pamoja na kunielezea dhamira ya Rais Magufuli, kuachia huru wimbo wangu, baada ya kuusikiliza kwa makini na kubaini hauna dosari ya kuufanya ufungiwe na mimi kunitia hatiani kama ilivyokuwa imechukuliwa na Jeshi la Polisi ambao waliniweka hadi rumande.
“Mwakyembe alisema kuwa rais amesikia wimbo wangu na kufurahishwa na mawazo yangu hivyo akaamua kumuagiza Over aniachie huru na wimbo uendelee kupigwa, ila aliomba kama kuna uwezekano nitunge wimbo mwingine ambao nitazungumzia mambo mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na juhudi za serikali.
“Zaidi alisema kuwa kama kuna uwezekano itabidi huu wimbo nifanye remix yake ambayo itanifanya niongeze mistari yenye kuzungumzia janga la madawa ya kulevya, wakwepa kodi na hata wale wote ambao wamekuwa wakipinga harakati za kiuchumi ikiwa sambamba na kuhujumu uchumi wetu.
“Waziri Mwakyembe, amenitaka pia niwe makini zaidi katika kazi yangu kwani nyimbo ambazo nimekuwa nikiimba hakika zimekuwa zikigusa moja kwa moja hisia za watu, jambo ambalo wengine wenye mioyo isiyokuwa na uvumilivu ni rahisi kushindwa kunivumilia na kujikuta wakitaka kunizuru moja kwa moja.
“Hakika nimefurahia ushauri wake na wawatu wengine kwani nikiwa katika ofisi zake niliweza kuongea pia na Naibu Waziri wa Kazi Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, ambaye pia aliniambia amekuwa akiheshimu na kuvutiwa sana na kazi zangu, hivyo naye kwa pamoja aliniambia niongeze umakini hasa kwenye tungo zangu ili siku moja zisiweze kuniingiza kwenye mitafaruku na watu.
“Kusema kweli wito wa Mwakyembe ulikuwa ni mzuri sana kwani umenipa mafunzo makubwa ya namna ya kuongeza ubunifu katika sanaa yangu, ila pia nimeweza kujifunza na kuwajua watu ambao sisi wasanii tumekuwa tukiwafikiria kama si wafuatiliaji wa kazi zetu, kumbe wao ndiyo wanasikiliza mstari kwa mstari.
“Nasema hivi kwa sababu wakati naongea na Mwakyembe alinigusia mistari kibao ya nyimbo zangu hata zile za nyuma jambo lililonishangaza na kunishitua kwani sikuwahi kutegemea kama angekuwa mfuatiliaji wa sanaa yetu kiasi cha kujua kila jambo, maana mimi hata kipindi anateuliwa nilikuwa namuona kama hataweza kusimamia kazi zetu kwa kuamini hajui chochote kwenye sanaa, kumbe sivyo hivyo.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Magufuli kwa wema wake alionionyesha, kwani amenijenga kwa kiasi kikubwa na kwamba nimefarijika kusikia akiusifia sana wimbo wangu kwani ni jambo linalotia moyo sana, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mwakyembe kwa kunionyesha kuwa anaitambua sanaa na anajua kila kitu kwenye tasnia hii, jambo ambalo naamini kupitia yeye tutazidi kunufaika na kazi zetu za muziki ambazo wengi wetu ndiyo ajira tulizojianzishia,”
“Hakika kupitia wimbo wangu huu nimepata elimu ambayo nitahakikisha naifikisha kwa Watanzania walio wengi ili siku moja niweze kuisaidia serikali yangu kuelimisha mambo muhimu ambayo kwa namna moja au nyingine huko nyuma sikujua kama serikali iko karibu na wasanii namna hii,” 
alisema Nay.

ASKOFU GWAJIMA ATISHIWA KIFO

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema ametishiwa kifo na kundi la watu asiowafahamu. Amesema kuwa watu hao waliomtumia ujumbe wa maandishi (SMS) kupitia simu yake ya mkononi na kuusambaza kwa watu, wengine walidai hatomaliza wiki hii iliyoanza leo.
Jana katika ibada yake, Gwajima alisema kuwa baada ya kuupata ujumbe huo alifanya maombi kwa ajili ya kuwafuta waliomtumia  na kujua nini chanzo cha vitisho hivyo.
“Kuna Askofu anajiita Nabii mdogo juzi alikuwa anasambaza meseji anasema naona Gwajima anamaliza mwendo wake, nimeapa kwa jina la bwana yeye anayesema nitamaliza mwendo kwa nguvu za giza atamaliza yeye kwanza na siyo mimi” alisema Gwajima
Aliongeza kuwa chombo cha Mungu hakiwezi kwenda mbinguni kabla hakijamaliza kazi ya Mungu na kwamba ataendelea kuishi hadi pale Mungu atakapoona imetosha na siyo kwa vitisho vya binadamu.
“Jana nilikuwa namsaka aliyetuma meseji hiyo kwenye makorido ya kiroho, nikamuona, mimi nina agano na Bwana kwamba adui zangu wakija kwa njia moja wataondoka kwa njia saba, silaha zote zitakazokuja kwangu hazitofanikiwa, yeye ndiye atakayekufa siku ile ile aliyoipanga, siyo mimi” alisema.
Alisema anawajua waliojiandaa kufanya uovu huo dhidi yake na kwamba haogopi chochote, kwani yeye ni sauti ya Mungu na ataendelea kufanya kazi kwa nguvu kama alivyoagizwa na Mungu ili kutimiza kusudi lake hapa duniani.
“Unasema Gwajima atakufa, najua mipango yako yote, nawajua wale watu uliowaandaa kwa ajili ya kuuwa wapo wapi, wana umri gani na wanafanya kazi gani. Huyu anachekesha  kweli, unataka Mungu akose sauti yake, watakufa wao waliotumwa na siyo mimi”
Gwajima alisema kuwa yeye na waumini wake wataendelea kuwa imara kwani wanamjua wanayemwamini na hawatishiwi na vitisho vya kifo kwa sababu Mungu atawashindia.

TABOA WASITISHA MGOMO WA MABASI

TABOA wasitisha mgomo baada ya makubaliano na Waziri Mbarawa ya kurekebisha mapungufu yaliyofanya watake kugoma ndani ya siku 14.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), leo imesema inayafanyia kazi madai yaliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) pamoja na Umoja wa Wasafirishaji wa Abiria jijini Dar es Salaam (UWADAR). Hii ni siku moja baada ya vyama hivyo kutoa tamko la kutaka kusitisha huduma ya usafirishaji kuanzia siku ya Jumanne.
Hata hivyo, SUMATRA kupitia Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johasen Kahatano imesema hakuna muswada wowote uliopelekwa bungeni wala suala la kusomwa kwa mara ya mwisho kwa muswada wa sheria inayotaka mmiliki wa gari kushitakiwa au kuhukumiwa kwa kosa alilofanya dereva.
“Hakuna kitu kama hicho, labda kama kuna kiongozi mwingine hapa katika mamlaka anayefahamu hilo, nitakupa namba ya simu ya Mkurugenzi Mkuu umuulize kama kuna jambo kama hilo,” alisema Kahatano.
Vilevile alisema kuwa hajui wamiliki wa mabasi walikozipata taarifa za muswada huo na leo SUMATRA inaweza kuangalia nini cha kufanya kabla ya kuanza kwa mgomo wa mabasi hayo.
Wamiliki wa mabasi walitangaza kusitisha huduma za usafirishaji kuanzia kesho jumanne ikiwa ni kwa lengo la kupinga sheria ya SUMATRA Sura ya 413 na ile ya Leseni za Usafirishaji Sura ya 317, inayotaka mmiliki wa gari kushtakiwa au kuhukumiwa kwa kosa alilofanya dereva.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu akisoma mapendekezo yaliyotolewa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho alisema mgomo huo siyo wa mabasi tu, unawahusu pia wasafirishaji wa malori pamoja na bajaji.
Hata hivyo wamiliki hao wa mabasi, leo walikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ujenzi mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kuhusiana na namna ya kuyafanyia kazi madai yao.
Mkutano huo wa Waziri Mbarawa na TABOA umefikia makubaliano kuwa mgomo usitishwe na madai yao kushughulikiwa ndani ya siku 14.

Jumapili, Aprili 02, 2017

TRUMP NA MPANGO WA KUIDHIBITI KOREA KASKAZINI

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Marekani itajiandaa yenyewe kuchukua hatua dhidi ya vitisho vya Nuklia vinavyoonyeshwa na Korea kaskazini.
Katika mahojiano na Gazeti la Financial Times, Trump amenukuliwa akisema ''kama China haitafanya chochote dhidi ya Korea kaskazini, sisi tutafanya''.
Majaribio ya makombora ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na Korea kaskazini, yatawaleta ana kwa ana kwa mara ya kwanza Trump na mwenzake wa China Xi Jinping.
kabla ya mkutano wa juma hili mjini Florida, washauri wa masuala ya usalama nchini Marekani wameelezwa kuharakisha kukamilisha orodha ya sera zilizopendekezwa.
Katika ziara yake ya kwanza katika bara la Asia, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rex Tillerson amesema diplomasia ya miaka 20 ya nchi za magharibi iliyolenga kuidhibiti Korea kaskazini imeshindwa.

PAPA FRANCIS ATAKA KUIMARISHWA AMANI DRC

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa wito wa kuimarishwa amani na utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo akitilia mkazo suala la kukomeshwa umwagaji damu katika mkoa uliozongwa na machafuko wa Kasai.
Papa Francis amesema kuwa, kunaendelea kutolewa ripoti na habari za mapigano ya umwagaji damu katika eneo la Kasai huko Congo DR ambayo yanawaathiri raia na kuwalazimisha wengine kuwa wakimbizi.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki amewataka wanadamu kuomba dua ya amani na kuwaombea wale wanaofanya jinai na mauaji hayo kuondoka katika utumwa wa chuki na ukatili.
Watu wasiopungua 400 wameuawa katika machafuko yanayoendelea kwa miezi kadhaa sasa katika mkoa wa Kasai ulioko katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 
Mkoa wa Kasai umekumbwa na ghasia tangu katikati ya mwezi Agosti, wakati askari wa kikosi cha serikali ya Congo walipomuua Kamwina Nsapu, aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo waasi dhidi serikali kuu Rais Joseph Kabila.
Wakati huo huo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetahadharisha kuwa ukatili unaofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa unaweza kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita. 
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Fatou Bensouda amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua na kuwapandisha kizimbani watu wanaohusika na uhalifu huo.