Jumatatu, Aprili 03, 2017

WALICHOKIZUNGUMZA NEY WA MITEGO NA MWAKYEMBE HIKI HAPA

Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, hatimaye amerejea kutoka Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma, ambapo alienda kuitikia wito wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison George Mwakyembe.
Hivi karibuni Nay alishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kuachia Wimbo wa Wapo uliokuwa na mashairi ya kuilenga serikali lakini baada ya siku chache Waziri Mwakyembe alitoa agizo la kuachiwa msanii huyo na wimbo huo kupigwa baada ya kusikilizwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli na kufurahishwa nao.

Baada ya Jeshi la Polisi kumuachia Nay, waziri alimuomba kufika Dodoma kukutana naye na kuzungumza mengi kuhusiana na sanaa. Over Ze Weekend limekuchambulia alichoambiwa;
“Nimeshaonana na Waziri Mwakyembe, kufuatia wito wake, ambapo nilifika hadi kwenye ofisi zake na tuliongea mambo mengi ikiwemo yeye kuniulizia kwa makini tungo yangu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa katika maongezi yetu alionekana akisifia sana kazi zangu.
“Kubwa zaidi aliloniambia yaani ikiwa pamoja na kunielezea dhamira ya Rais Magufuli, kuachia huru wimbo wangu, baada ya kuusikiliza kwa makini na kubaini hauna dosari ya kuufanya ufungiwe na mimi kunitia hatiani kama ilivyokuwa imechukuliwa na Jeshi la Polisi ambao waliniweka hadi rumande.
“Mwakyembe alisema kuwa rais amesikia wimbo wangu na kufurahishwa na mawazo yangu hivyo akaamua kumuagiza Over aniachie huru na wimbo uendelee kupigwa, ila aliomba kama kuna uwezekano nitunge wimbo mwingine ambao nitazungumzia mambo mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na juhudi za serikali.
“Zaidi alisema kuwa kama kuna uwezekano itabidi huu wimbo nifanye remix yake ambayo itanifanya niongeze mistari yenye kuzungumzia janga la madawa ya kulevya, wakwepa kodi na hata wale wote ambao wamekuwa wakipinga harakati za kiuchumi ikiwa sambamba na kuhujumu uchumi wetu.
“Waziri Mwakyembe, amenitaka pia niwe makini zaidi katika kazi yangu kwani nyimbo ambazo nimekuwa nikiimba hakika zimekuwa zikigusa moja kwa moja hisia za watu, jambo ambalo wengine wenye mioyo isiyokuwa na uvumilivu ni rahisi kushindwa kunivumilia na kujikuta wakitaka kunizuru moja kwa moja.
“Hakika nimefurahia ushauri wake na wawatu wengine kwani nikiwa katika ofisi zake niliweza kuongea pia na Naibu Waziri wa Kazi Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, ambaye pia aliniambia amekuwa akiheshimu na kuvutiwa sana na kazi zangu, hivyo naye kwa pamoja aliniambia niongeze umakini hasa kwenye tungo zangu ili siku moja zisiweze kuniingiza kwenye mitafaruku na watu.
“Kusema kweli wito wa Mwakyembe ulikuwa ni mzuri sana kwani umenipa mafunzo makubwa ya namna ya kuongeza ubunifu katika sanaa yangu, ila pia nimeweza kujifunza na kuwajua watu ambao sisi wasanii tumekuwa tukiwafikiria kama si wafuatiliaji wa kazi zetu, kumbe wao ndiyo wanasikiliza mstari kwa mstari.
“Nasema hivi kwa sababu wakati naongea na Mwakyembe alinigusia mistari kibao ya nyimbo zangu hata zile za nyuma jambo lililonishangaza na kunishitua kwani sikuwahi kutegemea kama angekuwa mfuatiliaji wa sanaa yetu kiasi cha kujua kila jambo, maana mimi hata kipindi anateuliwa nilikuwa namuona kama hataweza kusimamia kazi zetu kwa kuamini hajui chochote kwenye sanaa, kumbe sivyo hivyo.
“Nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Magufuli kwa wema wake alionionyesha, kwani amenijenga kwa kiasi kikubwa na kwamba nimefarijika kusikia akiusifia sana wimbo wangu kwani ni jambo linalotia moyo sana, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mwakyembe kwa kunionyesha kuwa anaitambua sanaa na anajua kila kitu kwenye tasnia hii, jambo ambalo naamini kupitia yeye tutazidi kunufaika na kazi zetu za muziki ambazo wengi wetu ndiyo ajira tulizojianzishia,”
“Hakika kupitia wimbo wangu huu nimepata elimu ambayo nitahakikisha naifikisha kwa Watanzania walio wengi ili siku moja niweze kuisaidia serikali yangu kuelimisha mambo muhimu ambayo kwa namna moja au nyingine huko nyuma sikujua kama serikali iko karibu na wasanii namna hii,” 
alisema Nay.

0 comments:

Chapisha Maoni