Jumatatu, Aprili 03, 2017

ASKOFU GWAJIMA ATISHIWA KIFO

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema ametishiwa kifo na kundi la watu asiowafahamu. Amesema kuwa watu hao waliomtumia ujumbe wa maandishi (SMS) kupitia simu yake ya mkononi na kuusambaza kwa watu, wengine walidai hatomaliza wiki hii iliyoanza leo.
Jana katika ibada yake, Gwajima alisema kuwa baada ya kuupata ujumbe huo alifanya maombi kwa ajili ya kuwafuta waliomtumia  na kujua nini chanzo cha vitisho hivyo.
“Kuna Askofu anajiita Nabii mdogo juzi alikuwa anasambaza meseji anasema naona Gwajima anamaliza mwendo wake, nimeapa kwa jina la bwana yeye anayesema nitamaliza mwendo kwa nguvu za giza atamaliza yeye kwanza na siyo mimi” alisema Gwajima
Aliongeza kuwa chombo cha Mungu hakiwezi kwenda mbinguni kabla hakijamaliza kazi ya Mungu na kwamba ataendelea kuishi hadi pale Mungu atakapoona imetosha na siyo kwa vitisho vya binadamu.
“Jana nilikuwa namsaka aliyetuma meseji hiyo kwenye makorido ya kiroho, nikamuona, mimi nina agano na Bwana kwamba adui zangu wakija kwa njia moja wataondoka kwa njia saba, silaha zote zitakazokuja kwangu hazitofanikiwa, yeye ndiye atakayekufa siku ile ile aliyoipanga, siyo mimi” alisema.
Alisema anawajua waliojiandaa kufanya uovu huo dhidi yake na kwamba haogopi chochote, kwani yeye ni sauti ya Mungu na ataendelea kufanya kazi kwa nguvu kama alivyoagizwa na Mungu ili kutimiza kusudi lake hapa duniani.
“Unasema Gwajima atakufa, najua mipango yako yote, nawajua wale watu uliowaandaa kwa ajili ya kuuwa wapo wapi, wana umri gani na wanafanya kazi gani. Huyu anachekesha  kweli, unataka Mungu akose sauti yake, watakufa wao waliotumwa na siyo mimi”
Gwajima alisema kuwa yeye na waumini wake wataendelea kuwa imara kwani wanamjua wanayemwamini na hawatishiwi na vitisho vya kifo kwa sababu Mungu atawashindia.

0 comments:

Chapisha Maoni