TABOA wasitisha mgomo baada ya makubaliano na Waziri Mbarawa ya kurekebisha mapungufu yaliyofanya watake kugoma ndani ya siku 14.
Wakati huohuo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), leo imesema inayafanyia kazi madai yaliyotolewa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) pamoja na Umoja wa Wasafirishaji wa Abiria jijini Dar es Salaam (UWADAR). Hii ni siku moja baada ya vyama hivyo kutoa tamko la kutaka kusitisha huduma ya usafirishaji kuanzia siku ya Jumanne.
Hata hivyo, SUMATRA kupitia Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara, Johasen Kahatano imesema hakuna muswada wowote uliopelekwa bungeni wala suala la kusomwa kwa mara ya mwisho kwa muswada wa sheria inayotaka mmiliki wa gari kushitakiwa au kuhukumiwa kwa kosa alilofanya dereva.
“Hakuna kitu kama hicho, labda kama kuna kiongozi mwingine hapa katika mamlaka anayefahamu hilo, nitakupa namba ya simu ya Mkurugenzi Mkuu umuulize kama kuna jambo kama hilo,” alisema Kahatano.
Vilevile alisema kuwa hajui wamiliki wa mabasi walikozipata taarifa za muswada huo na leo SUMATRA inaweza kuangalia nini cha kufanya kabla ya kuanza kwa mgomo wa mabasi hayo.
Wamiliki wa mabasi walitangaza kusitisha huduma za usafirishaji kuanzia kesho jumanne ikiwa ni kwa lengo la kupinga sheria ya SUMATRA Sura ya 413 na ile ya Leseni za Usafirishaji Sura ya 317, inayotaka mmiliki wa gari kushtakiwa au kuhukumiwa kwa kosa alilofanya dereva.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu akisoma mapendekezo yaliyotolewa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho alisema mgomo huo siyo wa mabasi tu, unawahusu pia wasafirishaji wa malori pamoja na bajaji.
Hata hivyo wamiliki hao wa mabasi, leo walikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ujenzi mawasiliano na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kuhusiana na namna ya kuyafanyia kazi madai yao.
Mkutano huo wa Waziri Mbarawa na TABOA umefikia makubaliano kuwa mgomo usitishwe na madai yao kushughulikiwa ndani ya siku 14.
0 comments:
Chapisha Maoni