Jumamosi, Aprili 15, 2017

POLISI MBEYA YAKAMATA WAHAMIAJI HARAMU 66 KUTOKA ETHIOPIA

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:- 
Mnamo tarehe 14.04.2017 majira ya saa 15:00 Alasiri huko katika Kijiji cha Simambwe kilichopo Kata na Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Mbeya Vijijini katika Barabara kuu ya Mbeya kuelekea Tukuyu Wilaya ya Rungwe, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 66 wote wanaume, umri kuanzia miaka 14 hadi 35 na wote raia wa nchini Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Wahamiaji hao walikamatwa baada ya Gari walilokuwa wakisafiria yenye namba za usajili T.913 AVM aina ya Fuso lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye PRINCE MATHEW (25) Mkazi wa Kijiji cha Kadia Mkoa wa Kilimanjaro kusimamishwa na askari wa usalama barabarani waliokuwa katika majukumu yao na kisha kufanya ukaguzi wa kawaida wa  gari hilo na ndipo waligundua kuwa gari hilo limebeba wahamiaji haramu.
Aidha baada ya kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu, dereva wa gari alihojiwa na kueleza kuwa aliwachukua watu hao kutoka eneo la Msata – Bagamoyo kwa ajili ya kuwapeleka Kasumulu Wilaya ya Kyela ili wavushwe kuelekea nchi jirani ya Malawi. 
Taratibu za kisheria zinafanyika ili wahamiaji hao wakabidhiwe Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria. Wakati huo huo, dereva wa gari PRINCE MATHEW anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kusafirisha wahamiaji haramu. Mahojiano zaidi yanaendelea ili kubaini na kuwakamata wahusika wote ikiwa ni pamoja na mtandao mzima wa wasafirishaji wa wahamiaji haramu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwafichua wahamiaji haramu na wahalifu kwa ujumla katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za siri zitakazofanikisha kukamatwa. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kusherehekea kwa amani na utulivu sikukuu ya Pasaka ikiwa ni pamoja na kifuata sheria za nchi na kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa aina yoyote. Pia anawataka wazazi na walezi kuwa makini hasa kwa watoto wadogo pindi waendapo maeneo yenye mikusanyiko kama vile kanisani.

0 comments:

Chapisha Maoni