Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis
ametoa wito wa kuimarishwa amani na utulivu katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo akitilia mkazo suala la kukomeshwa umwagaji damu
katika mkoa uliozongwa na machafuko wa Kasai.
Papa Francis amesema kuwa, kunaendelea kutolewa ripoti na
habari za mapigano ya umwagaji damu katika eneo la Kasai huko Congo DR
ambayo yanawaathiri raia na kuwalazimisha wengine kuwa wakimbizi.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki amewataka wanadamu kuomba dua ya amani na
kuwaombea wale wanaofanya jinai na mauaji hayo kuondoka katika utumwa
wa chuki na ukatili.
Watu wasiopungua 400 wameuawa katika machafuko yanayoendelea kwa
miezi kadhaa sasa katika mkoa wa Kasai ulioko katikati mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.
Mkoa wa Kasai umekumbwa na ghasia tangu katikati ya mwezi Agosti,
wakati askari wa kikosi cha serikali ya Congo walipomuua Kamwina Nsapu,
aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo waasi dhidi serikali kuu Rais Joseph
Kabila.
Wakati huo huo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetahadharisha
kuwa ukatili unaofanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwa
ni pamoja na mauaji ya wataalamu wawili wa Umoja wa Mataifa unaweza
kutambuliwa kuwa ni jinai ya kivita.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Fatou
Bensouda amesema kuwa hatasita kuwachukulia hatua na kuwapandisha
kizimbani watu wanaohusika na uhalifu huo.
0 comments:
Chapisha Maoni