Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17
maarufu kama Serengeti Boys, leo itapambana na Black Starlets ya Ghana
kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Katika mchezo huo utakaoanza saa 10.00 jioni,
Serengeti Boys itautumia kama ishara ya kuwaaga mamilioni ya
Watanzania kabla ya kusafiri kwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa
ya Afrika kwa vijana zitakazofanyika Gabon kuanzia Mei 14, mwaka huu.
Lakini kabla ya kutua Gabon, Serengeti Boys itakwenda Rabat, Morocco
kufanya kambi ya takribani mwezi mmoja kuanzia Aprili 5, mwaka huu.
Ikiwa huko angalau itacheza mechi za kirafiki zisizopungua mbili dhidi
ya wenyeji Morocco na timu nyingine ya jirani ama Tunisia au Misri.
Kambi hiyo ya Morocco itamalizika Mei mosi, mwaka hu ambako timu
itasafiri hadi Cameroon.
Ikiwa Cameroon, timu itacheza mechi mbili
za kirafiki za kimataifa dhidi ya wenyeji yaani Mei 3 na 6, mwaka huu
kabla ya kusafiri Mei 7, mwaka huu kwenda Gabon ambako Serengeti Boys
imepangwa kundi B pamoja na timu za Mali, Niger na Angola.
Vipimo
vya mechi dhidi ya Ghana kadhalika hapo baadaye Cameroon, vitakuwa
mwafaka kwenye kufanya tathmini ya uwezo wa Serengeti Boys kwani
wapinzani hao wamekuwa na rekodi nzuri kwenye soka la vijana na kwa
kipindi hiki zimepangwa kundi A pamoja na wenyeweji Gabon na Guinea.
0 comments:
Chapisha Maoni