Jumatano, Aprili 19, 2017

UHAKIKI WA VIBALI VYA UKAAZI SASA KIELEKTRONIKI

Serikali imezindua mfumo wa Kielektroniki wa Uhakiki wa Vibali vya ukazi “e-verification” hapa nchini ili kuongeza tija na kudhibiti upotevu wa mapato.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mfumo huo.
Akizungumzia mfumo huo Kamishna Jenerali Makakala amesema utasaidia Makampuni, Taasisi, Mashirika na watu binafsi kuhakiki vibali vya watumishi wao ili kuona kama ni halali ama si halali na idara hiyo itakuwa tayari kuwasaidia wale wote watakaokuwa na matatizo kupata ufumbuzi wa changamoto zao.
“Idara inatoa siku 90 kwa watu wote kuhakiki vibali vyao vya ukazi ili kama wana matatizo wasaidiwe kupata ufumbuzi” Alisisitiza Dkt Makakala.
Akizungumzia lengo la mfumo huo Makalala amesema utasaidia kuimarisha udhibiti wa wageni wanaoishi hapa nchini na kuzuia mianya ya upotevu wa maduhuli ya Serikali na mfumo huo ni rahisi na unatoa fursa kwa wageni wote wenye vibali vya ukaazi kuhakikiki kumbukumbu za vibali vyao ili kujua kama vimetolewa na Idara hiyo.
Aidha,Idara ya Uhamiaji inawaomba wadau wa huduma zake kufika wao wenyewe katika Ofisi zao katika ngazi ya Wilaya, Mikoa na Makao Makuu kwani huduma za Uhamiaji hazina uwakala.
Mfumo huo wa uhakiki wa vibali vya ukaazi kwa kutumia njia ya kielektroniki “e-verification” unapatikana kupitia tovuti ya uhamiaji ya www.immigration.go.tz.

0 comments:

Chapisha Maoni