Alhamisi, Aprili 27, 2017

ODINGA KUPEPERUSHA BENDERA YA UPINZANI KENYA

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA) umemteua aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka 2017.
Bw Odinga sasa atakabiliana na Rais Uhuru Kenyatta atakayetumia chama cha Jubilee kuwania muhula wa pili.
"Hii ni heshima kubwa sana ambayo ndugu zangu wamenifanyia, kwa kuniweka nipeperushe bendera ya NASA. Tumekuwa na vikao ambavyo vimechukua siku nyingi. Kila kitu tumeandika, tumekubaliana ya kwanza serikali tutakayoiunda, ambayo ni serikali ya mseto itakuwa ni serikali ya mpito," alisema Bw Odinga akihutubu baada ya kutangazwa kuwa mgombea.
Amesema atakuwa kama Joshua kwenye Biblia na kuvusha Wakenya hadi nchi ya ahadi.
"Sisi tuko kama timu, yenye pembe tano (Pentagon), wamenipa utepe wa nahodha, hiyo inaniunganisha mimi nao na Wakenya wote, tutatembea pamoja bega kwa bega. Tunataka kubadilisha Kenya na kutekeleza ndoto ya waanzilishi wa taifa letu".
Alisema serikali yake itaangazia kumaliza umasikini, kuimarisha afya, kuboresha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kurejesha gharama ya elimu na maisha chini.
Bw Odinga pia ameahidi kuhakikisha walimu na madaktari,pamoja na wafanyakazi wengine wanalipwa mishahara mizuri.
Kadhalika, ameahidi akishinda serikali yake itamaliza rushwa serikalini.
Makamu wa rais wa zamani Musalia Mudavadi amesema viongozi wote wakuu wa muungano huo wamekubalina kumuunga mkono mgombea huyo mmoja.
"Tumekubali kwamba mpangilio huu wa uongozi ni mpangilio ambao tunataka ulinganishwe na Rasimu ya Bomas ambayo Wakenya walitaka, lakini haikuidhinishwa," amesema.
Amesema mpango wao ni kuwa wadhifa wa kinara wa mawaziri na msaidizi wake, kama ilivyokuwa kwenye rasimu hiyo ya katiba.
Mgombea mwenza wa Bw Odinga atakuwa makamu wa rais wa zamani Bw Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Chama cha Wiper Democratic Movement.

0 comments:

Chapisha Maoni