Taasisi ya utafiti ya Gallup yenye makao yake
makuu mjini Washington Marekani imetangaza habari ya kuongezeka idadi
ya wananchi wa nchi hiyo walio na wasiwasi wa kupanda kiwango cha ukata
hasa kati ya watu wa pato la chini na tabaka la watu masikini nchini
humo.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na
taasisi hiyo kuanzia tarehe mosi hadi tarehe tano mwezi uliopita wa
Machi unaonesha kuwa, karibu asilimia 67 ya Wamarekani wenye kipato cha
chini wana wasiwasi mkubwa wa kukumbwa na umaskini mkubwa zaidi na
kupoteza makazi yao. Uchunguzi huo unaonesha kuweko ongezeko kubwa la
Wamarekani wenye wasiwasi wa kukumbwa na matatizo hayo ikilinganishwa na
miaka ya 2010 na 2011.
Uchunguzi wa huko nyuma wa maoni
ulionesha kuwa asilimia 51 ya raia wa Marekani walikuwa na wasiwasi wa
kuongezeka umaskini na kupoteza makazi yao.
Utafiti wa shirika la Gallup uliofanywa
mwaka 2014 nchini Marekani ulionesha kuwa idadi ya Wamarekani waliokuwa
na wasiwasi wa kupoteza makazi yao na kuongezeka umaskini wao
haikupindukia asilimia 35 wakati huo.
Machafuko, vitendo vya utumiaji mabavu,
uhalifu, jinai na ukosefu wa amani na usalama ni mambo mengine
yanayozifanya nyoyo za wananchi wa Marekani kuwa na wasiwasi mkubwa
hususan kati ya matabaka ya watu maskini na wenye kipato cha chini.
Matokeo ya uchunguzi wa hivi sasa wa
taasisi ya Gallup unaonesha kuwa Wamarekani wa matabaka yote wana
wasiwasi wa kupoteza makazi yao na kuongezeka umaskini na kwamba idadi
yao imeongezeka sana hivi sasa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
0 comments:
Chapisha Maoni