Katibu wa Jumuiya na Taasisi za KiislamuTanzania, amemtaka Rais John Pombe Magufuli kutimiza ahadi aliyoitoa kuwa atahakikisha kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Shein anamaliza tatizo la Zanzibar.
Sheikh Ponda Issa Ponda amesema Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, zinapinga kufanyika kwa uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar. Amesema jumuiya hiyo haioni sababu ya kurudiwa uchaguzi huo, kwani ulikuwa ni halali na taratibu zote zilifuatwa na matokeo yalikuwa halali. Wakati huo huo, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza) imelaani kauli ya Bakwata Mkoa wa Dar es Salaam ya kuunga mkono uchaguzi wa marudio wa Machi 20, uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha. Taarifa ya Jumaza imesema kuwa, jumuiya hiyo ilikuwa na uwakilishi katika uchaguzi aliofuta Jecha na kwamba, iliridhishwa na uchaguzi huo. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia katika mgogoro wa kisiasa baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura. Kwa mujibu wa tangazo la ZEC uchaguzi huo wa marudio utafanyika tarehe 20 ya mwezi ujao wa Machi. Chama cha wananchi CUF kimekwishatangaza kwamba, hakitashiriki uchaguzi huo wa marudio, kwani uchaguzi wa awali ulikuwa halali na mgombea wake Maalim Seif Sharif Hamad aliibuka mshindi.
0 comments:
Chapisha Maoni