Alhamisi, Februari 04, 2016

MADAKTARI NAO WATUMBULIWA MAJIPU IRINGA

WATUMISHI nane wa hospitali ya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwemo Mganga Mkuu, Dk Nelson Mtajwa wamesimamishwa kazi kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya kusababisha kifo cha mama mjamzito na mtoto wake aliyefariki kabla hajifungua hospitalini hapo, mjini Mafinga.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Shaib Nnunduma amekiri kusimamishwa kazi kwa watumishi hao na kwamba hatma yao itategemea matokeo ya uchunguzi huo.
Mbali na Dk Mtajwa, wengine waliosimamishwa kazi kwa mujibu wa mkurugenzi huyo ni pamoja na Prosper Kalinga, Greysoni Sanga, Ajue Kilingatu, Jackilini Mtavangu, Miraji Ngule, Sixter Nyenza, pamoja na dobi wa hospitali hiyo Nelson Nyenza.
Kusimamishwa kazi kwa watumishi hao kumekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kuunda timu ya uchunguzi iliyoyopewa jukumu la kufuatilia malalamiko ya wagonjwa dhidi ya baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo wanaotuhumiwa kufanya kazi kwa mazoea huku wakitumia lugha zisizofaa kwa wagonjwa.
Nnunduma alisema tayari watumishi hao wameandikiwa barua za kujielezea kuhusiana na tuhuma zinazowakabili ikiwemo ya kusababisha kifo cha mjamzito huyo.

0 comments:

Chapisha Maoni