Jumamosi, Februari 06, 2016

WATOTO 7200 HUFIA TUMBONI KILA MWAKA

Utafiti uliotolewa kwenye jarida la “The Lancet” la Uingereza unaonesha kuwa hivi sasa kila mwaka watoto milioni 2.6 wanafia tumboni, hii inamaanisha kila siku watoto 7200 hivi wanafia tumboni duniani, na nusu ya watoto hao wanafariki wakati wa kujifungua.
Maana ya watoto kufia tumboni ni kuwa watoto wanafariki katika muda unaoanzia wiki 28 tangu mwanamke apate mimba hadi wakati wa kujifungua. Utafiti unaonesha kuwa kutoka mwaka 2000 hadi 2015, ingawa idadi ya watoto wanaofia tumboni imepungua kwa kiasi kidogo duniani, lakini vifo vingi bado vinatokea katika nchi zenye pato la wastani au la chini.
Utafiti huo unaonesha kuwa kupitiliza muda wa kujifungua ni chanzo kikuu cha watoto kufia tumboni. Pili ni matatizo ya kiafya ya wajawazito, kama vile, ukosefu wa virutubisho, mtindo mbaya wa maisha, ukiwemo unene na uvutaji wa sigara, na maradhi mbalimbali yakiwemo ugonjwa wa kusukari, ugonjwa wa mishipa ya damu ya moyo. Tatu ni maradhi ya kuambukiza pamoja na ugonjwa wa malaria. 
Mbali na hayo, umasikini pia ni chanzo muhimu cha vifo vya watoto. Kiwango cha watoto wanaofia tumboni kusini mwa jangwa la Sahara ni cha juu zaidi kuliko sehemu nyingine duniani.

0 comments:

Chapisha Maoni