Jumamosi, Februari 06, 2016

BURUNDI YATUHUMIWA KUANDAMA WAPINZANI TANZANIA

Wakimbizi kutoka Burundi ambao wametorokea katika nchi jirani ya Tanzania wameituhumu serikali ya Bujumbura kuwa inatuma watu waliojizatiti kwa silaha kwenda kukabiliana na wafuasi wa upinzani miongoni mwao katika kambi za wakimbizi za Tanzania.
Kanali ya Televisheni ya Al-Jazeera imeripoti kuwa, wakimbizi raia wa Burundi wamesema kuwa maisha yao yamo hatarini katika kambi hizo, wakidai kuwa serikali ya Rais Pierre Mkurunziza inayatuma makundi ya wabeba silaha kwenda kuwahujumu. Zaidi ya Warundi laki mbili wameikimbia nchi yao tangu nchi hiyo itumbukie katika mgogoro mpya wa kisiasa Aprili mwaka jana, huku asilimia 50 ya idadi hiyo ikikisiwa kuwa imekimbilia Tanzania. Hii ni katika hali ambayo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, amesema baadhi ya askari waasi wa Burundi, wamebainika kukimbia nchini na kuanza kushawishi vijana wajisajili ili wajiunge na vikundi vya waasi. Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akifunga Mkutano wa Pili wa Bunge mjini Dodoma na kuwataka wakimbizi na wananchi, kushirikiana na vyombo vya usalama, kutoa taarifa za uhalifu. Majaliwa amesema: “Kutokana na ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.“ Hata hivyo Waziri Mkuu wa Tanzania amesisitiza kuwa, pamoja na changamoto hiyo, ambapo kambi za wakimbizi zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895; kutoka mataifa ya Burundi (156,377), Congo-DRC (62,176), Somalia (150) na mataifa mchanganyiko (192) ikiwemo Rwanda, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia, hali ya usalama katika nchi hiyo kwa ujumla ni shwari.

0 comments:

Chapisha Maoni