Jumapili, Februari 07, 2016

KUENDELEA MAAMBUKIZI YA VIRUSI VYA UGONJWA HATARI WA ZIKA

Virusi vya ugonjwa hatari wa Zika vinaendelea kutapakaa. Ripoti ya hivi karibuni ya Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), imetahadharisha juu ya kuenea zaidi maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Zika katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.
Rena Sidani, msemaji wa shirika hilo katika eneo la Mashariki ya Kati amesema kuwa, nchi saba ambazo ni Misri, Saudi Arabia, Sudan, Yemen, Somalia, Pakistan na Djibouti, zinakabiliwa na hatari ya kuambukizwa virusi hivyo hatari vya Zika. Sidani ameongeza kuwa, mbu wanaobeba virusi vya ugonjwa huo, wanaelekea katika nchi hizo suala ambalo linaonyesha kuwepo uwezekano wa kuenea maradhi hayo katika nchi hizo. Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), amezitaka nchi hizo kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo. Kabla ya hapo pia WHO lilikuwa limetahadharisha juu ya kuenea ugonjwa huo katika nchi za Ulaya.
Kufuatia kuripotiwa kesi ya ugonjwa wa Zika nchini Marekani, Jumatano iliyopia WHO sanjari na kutahadharisha juu ya uwezekano wa kuenea virusi vya maradhi hayo katika nchi za Ulaya katika msimu wa machipuo na joto, imewataka viongozi wa nchi hizo kuchukua hatua za lazima kuhusiana na suala hilo.
Suzana Yacob, Msimamizi wa Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Ulaya, ametangaza kuwa hadi sasa hakuna chanjo iliyokwishapatikana kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya virusi vya homa ya Zika, na amewataka viongozi wa nchi za bara hilo kuchukua hatua madhubuti kwa lengo la kuzuia viini vya maambukizi ya ugonjwa huo. Ameongeza kuwa, hadi sasa idadi kubwa ya waathirika wa virusi wa maradhi hayo wamesafiri katika nchi za Ulaya na kwamba kutokana na mazingira yasiyoridhisha, mbu wa ugonjwa huo, bado hawajaanza kueneza virusi hivyo.
Jana viongozi wa Idara za Afya na Matibabu nchini Italia waliripoti kesi tisa za maambukizi ya virusi vya Zika nchini humo. Kwa mujibu wa viongozi wa Italia, kesi nne kati ya hizo tisa zimeripotiwa katika mji wa Veneto, kaskazini mwa nchi hiyo na kwamba waathiriwa hao wanaendelea kupata matibabu katika vituo vya afya, baada ya kufanya safari huko Amerika ya Kusini na eneo la Caribbean.
Sanjari na WHO kutangaza hali ya hatari duniani kutokana na kuenea virusi hivyo vya Zika, limetangaza kuwa limeunda idara maalumu ya majanga duniani kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo. Anthony Costello, mmoja wa wataalamu wa WHO amesema kuwa, katika idara hiyo watahudhuria wafanyakazi wa WHO kutoka maeneo tofauti ya dunia ili kutoa radiamali yao ya pamoja dhidi ya maradhi hayo ya Zika. Ameongeza kuwa, idara hiyo ya majanga itatumia uzoefu uliopatikana kutokana na ugonjwa wa Ebola.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), zaidi ya watu milioni nne ndani ya nchi 21 za Amerika, wamekumbwa na virusi hivyo.
Ugonjwa wa Zika unaambukizwa kupitia wadudu na unaweza kuambukizwa kupitia mbu aina ya mbu wa Aedes. Mbu huyo pia mbali na virusi vya ugonjwa huo, wanaweza kueneza aina nyingine ya virusi vya maradhi mengine kama vile homa ya manjano, homa ya dengue na ugonjwa wa chikungunya.

0 comments:

Chapisha Maoni