Waziri wa Ulinzi wa Tunisia ametangaza kuwa nchi hiyo itaweka uzio wa umeme katika mpaka wa nchi hiyo na Libya ili kukabiliana na tishio la makundi ya kigaidi.
Farhat al Horchani Waziri wa Ulinzi wa Tunisia ameongeza kuwa wataalamu wa kijeshi wa Ujerumani na Marekani watatoa mafunzo kwa jeshi la Tunisia kuhusu namna ya kutumia uzio huo.
Jeshi la Tunisia hivi sasa limeshajenga kanali moja na ukuta wenye urefu wa kilomita 200 katika eneo la mpakani la Sabkha al Ain na hivi karibuni pia linatarajia kuweka uzio wa umeme katika eneo la mpaka kati ya nchi hiyo na Libya.
Waziri wa Ulinzi wa Tunisia amesema kuwa, ujenzi wa ukuta huo wa mpakani kutoka katika eneo la Ras al Jadir hadi al Dhahabiya kusini mwa nchi hiyo tayari umekamilika na kwamba utasaidia kuzuia kuingia magaidi. Waziri wa Ulinzi wa Tunisia ameongeza kuwa maelfu ya Watunisia ni wanachama wa kundi la Daesh huko Libya na wengi wa magaidi hao waliwasili Syria na Libya baada ya kushtadi mashambulizi dhidi ya kundi hilo la kigaidi.
Imetabiriwa kuwa katika miezi ijayo nchi za nje zitaanzisha mashambulizi huko Libya, suala ambalo limeitia wasiwasi Tunisia. Tunisia imetaka kuwepo mawasiliano kati yake na Libya kabla ya kuanza oparesheni hizo za kijeshi.
0 comments:
Chapisha Maoni