Jumamosi, Februari 06, 2016

MUGABE ATANGAZA BAA LA NJAA ZIMBABWE

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ametangaza baa la njaa linaloisumbua nchi yake kuwa janga la kitaifa.
Nchi hiyo haijapata mvua za kutosha tangu mwaka jana na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu milioni 1.5 wanahitaji msaada wa chakula.
Tangazo hilo la Rais Mugabe limetolewa siku chache tu baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kumhimiza atangaze baa hilo kuwa janga la kitaifa ili mashirika ya kimataifa ya misaada yaweze kuchangisha pesa haraka za kusaidia raia wa Zimbabwe. Hata hivyo serikali imewataka raia kutoingiwa na wasiwasi ikisema kuna mkataba wa kununua tani nyingi za mahindi kutoka Zambia.
Itakumbukwa kuwa, Oktoba mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulitoa ombi la dharura la dola milioni 86 kwa ajili ya chakula cha msaada kwa Zimbabwe.
Sekta ya kilimo ndiyo iliyoathirika sana huku wakulima wa tumbaku na pamba wakikosa mavuno. Maelfu ya mifugo pia imeangamia kutokana na ukame wa muda mrefu nchini Zimbabwe.
Rais Mugabe amesema madhila yanayowakumba wananchi wake yanatokana na vikwazo vya kidhulma vya nchi za Magharibi dhidi ya Zimbabwe.

0 comments:

Chapisha Maoni