MSANII nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond
Platnumz’ huenda akaingia matatani baada ya juzi kupanda jukwaani
kutumbuiza katika Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.
Tangu msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi wao
kujiuliza nini maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au
la, hasa ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa
wasanii na wengineo kutotumia mavazi hayo.
Mbali ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa wakiwa
katika mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya
nyimbo zake, Ney wa Mitego.
Wakati shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza kumzomea
kila alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa hilo
kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa
amevaa mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika
katika bastora na baadaye katika bunduki ya kivita.
Kitendo hicho, kilionekama kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi na
mashabiki wa muziki waliokuwa wamejazana katika viwanja vya Leaders
Club, huku kila mmoja akiwa na tafsiri yake.
Baada ya tukio hilo la juzi usiku, kitendo cha nyota huyo kuvalia
mavazi hayo ya JWTZ, kimeibua mjadala hadi katika mitandao ya kijamii
kuanzia jana asubuhi, ambapo picha za msanii huyo zikitumika kujenga
hoja ya uhalali wa kufanya hivyo, huku vijana kadhaa wanaokutwa nazo
mitaani wakiteswa vibaya na jeshi hilo.
Kwa upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa wake wa
Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika
shoo hiyo.
Tanzania Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni,
Camilius Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa hajui
chochote na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na
wasaidizi wake.
Alipotafutwa Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu yake
iliita bila kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata
taarifa na kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake
anaweza kulizungumzia hilo.
Tukio hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana mmoja
aliyekuwa amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es
Salaam, kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji
machafu yaliyotuama.
Aidha, msanii Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ aliwahi kuhojiwa na Jeshi
hilo kwa kutumia mavazi ya kijeshi katika kibao chake cha Simba wa
Afrika, ambapo alijitetea pamoja na kuomba msamaha kwa kilichofanyika.
Kutokana na wimbi la watu mbalimbali hasa wasanii kuvalia mavazi
yanayofanana na sare za jeshi hilo, hivi karibuni Kurugenzi ya Habari na
Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ, ilionya kama ifuatavyo:
Kumejitokeza kama fasheni kwa baadhi ya wasanii, hasa wanamuziki wa Bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.
Inawezekana kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo hawafahamu ni kinyume cha sheria ya nchi kukutwa nazo, ingawa kutokujua sheria bado sio utetezi mbele ya mahakama.Mtu yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi, atakuwa ametenda kosa, kwa hiyo atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.Katika uvaaji au uingizaji nguo, kama itatokea kwamba nguo hizo zinafanana kwa aina yoyote ile na zile za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ikadhaniwa kuwa ni hizo, mtu huyo ana hatia na anastahili kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo
ilifafanua taarifa hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni