Fundi radio maarufu mjini hapa, Daniel Mosha (53), amefariki dunia
wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa baada ya kuugua
ghafla akiwa anafanya mapenzi na mwalimu mmoja katika nyumba ya kulala
wageni iitwayo Cheyo. Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 11:00 alfajiri katika nyumba
hiyo iitwayo Cheyo chumba namba nne, wakati fundi huyo akijivinjari na
mpenzi wake huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi
(SACP), Geofrey Kamwela, alisema fundi huyo alifariki Oktoba 14 mwaka
huu saa 10.30 jioni katika hospitali ya Mkoa alikokimbizwa baada ya
kuzidiwa akiwa gesti.
Aidha, Kamanda Kamwela alisema kuwa Oktoba 13 mwaka huu majira ya
jioni, marehemu akiwa nampenzi wake wa muda mrefu, Serafine Lucian (56),
mwalimu wa shule ya Msingi Manguanjuki manispaa ya Singida, walipanga
chumba namba nne kwa ajili ya mapumziko ya usiku mzima.
Ilipofika alfajiri saa saa 11 Oktoba 14 mwaka huu, mwanaume huyo alianza kuugua ghafla huku akikoroma na ndipo mwalimu Serafine, aliamka na kumwita meneja wa nyumba hiyo na kumweleza juu ya hali ya mpenzi wake
alisema.
Alisema meneja pamoja na mwalimu huyo, walifanya juhudi za kumkimbiza
hospitali ya Mkoa ili kuokoa maisha yake lakini mambo yaliendelea kuwa
magumu.
Hata hivyo, Kamanda Kamwela, alisema uchunguzi wa awali unaonyesha
kuwa katika chumba walichopanga wapenzi hao, pamoja na vitu vingine
zilikutwa paketi tupu za pombe kali aina ya viroba vilivyotumika.
Tunaendelea na uchunguzi ili kujua kama kuna mtu au watu wanaohusika na kifo hicho cha fundi radio, lakini tunamshikilia mwalimu huyo kwa uchunguzi zaidi, ili pamoja na mambo mengine kuchunguza iwapo kuna mtu au watu waliohusika na kifo hicho
alisema Kamwela.
0 comments:
Chapisha Maoni