Alhamisi, Agosti 28, 2014

HABARI MBAYA KUHUSU BUNGE MAALUM LA KATIBA

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam imeanza mchakato wa kusikiliza kesi dhidi ya Bunge la Katiba baada ya kupanga jopo la majaji wa kuisikiliza.
Kesi hiyo namba 28 ya 2014, ilifunguliwa mahakamani hapo na mwandishi wa habari, Saed Kubenea kupitia kwa Wakili Peter Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hilo.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka mahakamani hapo jana na kuthibitishwa na Wakili Kibatala, kesi hiyo imepangwa kusikiliza na jopo la majaji watatu.
Majaji hao ni Agustine Mwarija ambaye ndiye kiongozi wa jopo akishirikiana na Dk Fauz Twaib na Aloysius Mujulizi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vyetu, licha ya kesi hiyo kupangiwa jopo la majaji hao, hadi jana ilikuwa haijapangwa tarehe ya kutajwa.
Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba Namba 83 ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda yaliyopewa namba 29 ya 2014 na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge, yote yalifunguliwa mahakamani hapo chini ya hati ya dharura.
Katika maombi ya msingi, Kubenea anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati hiyo, uamuzi wa kufungua kesi hiyo kuomba tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge umetokana na mjadala na mvutano wa kisheria ndani na nje ya Bunge hilo kuhusu mamlaka ya chombo hicho.

0 comments:

Chapisha Maoni