Jumatano, Julai 02, 2014

MPAKA SASA EBOLA IMEUA 467

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuwa kufikia Juni 30, idadi ya vifo vilivyotokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola imepanda na kufikia watu 467, huku kesi za maambukizi ya virusi hivyo hatari katika nchi tatu zilizoathiriwa za Guinea Conakry, Liberia na Sierra Leone zikiwa 759.
Idadi kubwa zaidi ya vifo hivyo imetokea nchini Guinea, ambako watu 303 wamefariki dunia, huku Liberia ikishuhudia vifo 65 na vifo 99 kutokea Sierra Leone.
Kwa mujibu wa WHO, sababu tatu kubwa zinazochangia kuongezeka maambukizi katika ukanda huo ni utamaduni na imani za kijadi vijijini, idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyo nje ya miji ya Conakry na Monrovia, pamoja na shughuli za kibiashara na kijamii zinazoendelea kwenye mipaka ya nchi hizo na watu kuvuka mipaka. WHO imesema kudhibiti mlipuko huo kunahitaji hatua kubwa katika nchi hizo, hususan kwenye maeneo ya mipaka.
Kama njia ya kufuatilia tatizo hilo, WHO inaandaa mkutano wa siku mbili wa ngazi ya juu kwa ukanda huo kuanzia leo Julai pili mjini Accra, Ghana, ili kutathmini hali, kutambua upungufu, kubuni mpango wa kuudhibiti ugonjwa huo, pamoja na kuzidisha utashi wa kisiasa na ushirikiano mipakani baina ya serikali za ukanda huo.

0 comments:

Chapisha Maoni