Jumatano, Julai 02, 2014

UTABIRI WA VIFO VYA MASTAA WAMUANGUKIA AUNT EZEKIEL...AJILILIA

SIKU chache baada ya Nabii wa Huduma ya Ufufuo, Buza jijini Dar, Yaspi Paul Bendera kutabiri kuwa vifo vya mastaa vitaendelea, staa wa sinema Bongo, Aunt Ezekiel amemwaga machozi baada ya kuhusishwa kuwa yeye ndiye anayefuata kufa.
Kupitia gazeti la Ijumaa, Juni 13, mwaka huu, Nabii Bendera alisema ameoneshwa kwamba wasanii 20 wangekufa hivyo kama wanataka kujinusuru, wafike kanisani kwake na kupakwa mafuta.
Wakati gazeti hilo lilipoingia mtaani, ukurasa wa mbele uliambatanisha picha mbalimbali za baadhi ya wasanii waliofariki pamoja na wengine ambao wapo hai akiwemo Aunt Ezekiel (pichani) ndipo utata ulipoanzia.
Chanzo kilicho karibu na staa huyo, kilipenyeza habari kuwa, ndugu zake walimpigia simu Aunt ambapo walionesha kuwa na hofu ya kifo ambayo ilimfanya mwigizaji huyo naye aangue kilio mara kwa mara.
Ndugu zake walilia sana kwani baada ya kuona picha ya Aunt katika gazeti, waliamini maneno ya nabii huyo kwa kujua pengine anayefuata kufa kati ya hao kumi ni ndugu yao.
Aunt alilia sana siku hiyo na Wema (Sepetu) ndiye alisimama kumsihi asiendelee lakini kama haitoshi, bado amekuwa akiteseka mara kwa mara kila anapokumbuka tu, anakosa amani na kujikuta analia.
kilisema chanzo.
Hata hivyo, chanzo kimeeleza kuwa baada nguvu kubwa kutoka kwa marafiki wa karibu wa Aunt akiwemo Wema wamekuwa wakimsihi amuombe Mungu kwani si kwamba picha yake kutumika gazetini ndiyo atakufa wala maneno ya nabii huyo si sababu ya kuamini kwamba kweli vifo hivyo vitatokea.
Wamemtaka amuombe Mungu na kutosikiliza maneno ya watu maana kuna watu ambao wamekuwa wakishadadia ishu hiyo katika mitandao na kumfanya Aunt aingiwe na hofu ya kifo, kidogo ameanza kuwaelewa
kilisema chanzo.
Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimtafuta Aunt, alipopatikana aliweka wazi kuwa suala hilo limemkosesha amani sana pamoja na ndugu zake.
Walijua ndiyo nakufa, na mimi pia niliposikia harakaharaka niliamini nimetajwa mimi hususan waliponiambia picha yangu imetumika gazetini, nililia sana siku hiyo na siku zilizofuata pia watu walizidi kuniliza mitandaoni, mwisho wa siku nimemwomba Mungu anisimamie, atakaponichukua ni kwa mapenzi yake kama maandiko yanavyosema
alisema Aunt.
Kwenye utabiri huo, nabii huyo alinukuliwa kuwa ndani ya mwezi Juni, idadi ya wasanii 20 wangefariki lakini hadi sasa hakuna kifo chochote kilichotokea hali ambayo inawafanya baadhi ya watu kuamini kwamba masuala ya kifo ni Mungu pekee anayejua nani atakufa lini.

0 comments:

Chapisha Maoni