Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuwa kufikia Juni 30,
idadi ya vifo vilivyotokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola imepanda na
kufikia watu 467, huku kesi za maambukizi ya virusi hivyo hatari katika
nchi tatu zilizoathiriwa za Guinea Conakry, Liberia na Sierra Leone
zikiwa 759.
Idadi kubwa zaidi ya vifo hivyo imetokea nchini Guinea, ambako watu
303 wamefariki dunia, huku Liberia ikishuhudia vifo 65 na vifo 99
kutokea Sierra Leone.
Kwa mujibu wa WHO, sababu tatu kubwa zinazochangia kuongezeka
maambukizi katika ukanda huo ni utamaduni na imani za kijadi vijijini,
idadi kubwa ya watu katika maeneo yaliyo nje ya miji ya Conakry na
Monrovia, pamoja na shughuli za kibiashara na kijamii zinazoendelea
kwenye mipaka ya nchi hizo na watu kuvuka mipaka. WHO imesema kudhibiti
mlipuko huo kunahitaji hatua kubwa katika nchi hizo, hususan kwenye
maeneo ya mipaka.
Kama njia ya kufuatilia tatizo hilo, WHO inaandaa mkutano wa siku
mbili wa ngazi ya juu kwa ukanda huo kuanzia leo Julai pili mjini Accra,
Ghana, ili kutathmini hali, kutambua upungufu, kubuni mpango wa
kuudhibiti ugonjwa huo, pamoja na kuzidisha utashi wa kisiasa na
ushirikiano mipakani baina ya serikali za ukanda huo.
0 comments:
Chapisha Maoni