Jumatano, Julai 02, 2014

PASSPORT ZA KUSAFIRIA KUBADILISHWA

IDARA ya Uhamiaji inatarajia kubadilisha pasi za kusafiria zitakazokuwa na alama zaidi za utambuzi.
Akizungumza katika banda la idara hiyo lililopo kwenye maonyesho ya 38 ya kimataifa ya biashara Dar es Salaam (DITF), Ofisa Uhusiano wa Uhamiaji, Tatu Burhan, alisema kuwa bajeti ya mwaka 2014/15 itatumika kubadilisha pasi hizo.
Tatu alisema kuwa mabadiliko hayo yataanza rasmi mwaka 2015 na pasi mpya zitakuwa na alama zaidi za utambuzi.

Passport tutakayobadili ni ya awamu ya nne, na itakuwa na alama nyingi zaidi za kiutambuzi za kimataifa na tunafanya hivyo ili kukabiliana na watu wasio waaminifu lakini pia ni kuweka usalama zaidi na kuondoa wimbi la uharamia wa passport
alisema.
Aliongeza kuwa katika maonyesho hayo watakuwa wakitoa pasi za kusafiria kwa waombaji wapya waliokamilisha vigezo.
Ubadilishwaji huo utakuwa wa nne baada ya kufanyika mwaka 1961, 1992 na 2005.
Wakati huo huo, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), umewataka Watanzania walio katika sekta zisizo rasmi kujiunga na Mpango wa Uchangiaji wa Hiari (PSS) ili kujiwekea akiba ya baadaye.
Akizungumza jana, Ofisa Masoko wa PSPF, Magira Werema, alisema kuwa mpango wa PSS utamsaidia mjasiriamali wa kawaida kujiwekea akiba ya baadaye.
Alisema kuwa mpango huo utamwezesha mwanachama kupata mafao mbalimbali pamoja na mkopo wa nyumba.
Werema alisema kuwa wajasiriamali watapata fursa ya kujiunga moja kwa moja ili wajiwekee akiba itakayowapa faraja baadaye.
Mchangiaji wa hiari atatakiwa kuchangia kwa miaka mitano na atapewa mkopo wa nyumba au anaweza akakopa kwa njia ya upangaji na atalipa kila mwezi
alisema.
Pia alisema kuwa kwa sasa wanajipanga kutoa fao la uzazi kwa wanachama wanawake waliochangia miezi 24 kwa kulipa asilimia 130 ya mshahara wake.
Nayo Benki ya NMB imeanzisha mkopo wa pikipiki na bajaji ili kuhakikisha Watanzania wanapata nafuu ya usafiri na kutoa ajira kwa vijana.
Ofisa Mikopo wa NMB, Donatila Wapalila, alisema mikopo hiyo itatolewa kwa Watanzania wote waliofikisha miaka 18 na italipwa kwa muda wa miaka miwili.
Domitila alisema kuwa NMB imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania anamiliki bajaji na kujikomboa kiuchumi.
Katika mkopo huo, pia tutawapa huduma ya bima ambapo tumejiunga na reliance kwa kutoa bima kubwa na bima ya maisha kwa miaka miwili
alisema.
Aliongeza kuwa mkopo huo wa gharama nafuu unapatikana katika matawi yote ya benki hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni