KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya (RPC), Ahmed Msangi, amemwagiza Mkuu
wa Polisi (OCD) Wilaya ya Mbarali, Julius Lukindo kumkamata
mfanyabiashara Tanu Deminyembe anayedaiwa kupora magunia 450 ya mpunga.
Agizo la kamanda huyo limekuja baada ya uchunguzi wa Tanzania Daima
kwa wiki nne kuhusu mfanyabiashara Tanu Deminyembe kuliagiza kundi lake
na kwenda kupora mpunga kwa wakulima aliowakopesha fedha kinyume cha
mkataba.
Kugundulika kwa mvutano huo kulitokana na mfanyabiashara huyo
kuwekeana mikataba na wakulima msimu wa kilimo ili wanapoanza mavuno
wamrejeshee magunia ya mpunga na aina ya mbegu anayoihitaji.
Ili kukamilisha biashara hiyo, George Mwanga aliangukia kwenye mikono
ya Tanu aliyemkopesha sh milioni mbili na kutakiwa arejeshe magunia 58
ya mpunga aina ya saro baada ya mavuno.
Habari zaidi zinabainisha kwamba mkulima huyo aliporwa magunia mengi
ya mpunga kinyume cha mkataba uliopaswa kumalizika jana huku
akishuhudia kundi la vijana wakiongozwa na Mwangosi kuingia shambani na
kubeba mpunga huo wakidai kuagizwa na bosi wao.
Mwanga alilithibitishia gazeti hili kuwa uporaji ulifanywa shambani kwake na kuchukuliwa magunia yote wakimuacha hana kitu.
Huu ni uporaji, kweli kanikopesha fedha kwa mkataba huu unaouona, hakupaswa kuwatuma watu kuja kuchukua mpunga wangu kabla ya wakati… wamechukua hata mali isiyowahusu, nimekimbilia polisi sijui watanisaidiaje
alisema Mwanga.
Tanu alikiri kumkopesha fedha mkulima huyo na kudai kuwa alichukua
magunia 86 ya mpunga kabla ya wakati wa mkataba huku akikana kulituma
kundi hilo kwenda kuchukua mpunga.
Huyu mzee alinipigia simu kipindi anataka hela, hao waliokwenda kuchukua mpunga shambani kwake siwafahamu… nilipokuwa Dar aliniomba nimuongezee fedha hata kwa riba mimi nilikataa. Niliporudi nilichukua magunia 86, bado magunia 54 namdai
alisema Tanu.
Kamanda Lukindo alipohojiwa kuhusu uporaji huo, alidai hana taarifa
na kumtaka mkulima aliyefanyiwa kitendo hicho afike ofisini ambako
alimkutanisha na mfanyabiashara huyo kwa lengo la kuwashauri
wamalizane.
Sakata hilo lilifika kwa Kamanda Msangi ambaye baada ya kuhojiwa
alimuagiza OCD Lukindo kuwakamata waliohusika na uporaji huo na
kuwafungulia kesi ya jinai ili kuliepusha jeshi hilo kuchafuka kwa
madai ya kushindwa kufanya kazi.
Habari zilizothibitishwa na Tanzania Daima kutoka Mbarali, ni kwamba
mfanyabiashara huyo amekamatwa na msako unaendelea kuwanasa vijana
waliochukua magunia 450 ya mpunga.
0 comments:
Chapisha Maoni