Mahakama kuu ya Tanzania imetupilia mbali kesi dhidi ya waziri mkuu,
Mh. Mizengo Pinda iliyofunguliwa na kituo cha sheria na haki za binadamu
LHRC na chama cha wanasheria Tanganyika TLS kwa sababu hawana mamlaka
kisheria ya kumshtaki.
Kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na jopo la majaji
watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakih Jundu imetupiliwa mbali baada
ya jopo hilo kukubaliana na hoja za pingamizi zilizowasilishwa na Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju.
Kituo cha sheria na haki za binadamu na TLS
walimshtaki Waziri Mkuu Pinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
kauli aliyoitoa bungeni Juni 20 mwaka jana ya kuwataka polisi kuwapiga
watakaokaidi amri halali ya polisi.
Akisoma hukumu hiyo jaji Jundu huku akinukuu baadhi
ya ibara amesema Ibara ya 100 (2) inaweza kujadiliwa mahakamani, ambayo
inasema bila kuathiri katiba au masharti ya sheria nyingine yoyote
inayohusika, Mbunge yoyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai
mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya
Bunge au alilolileta bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au
vinginevyo.
Amesema kutokana na sababu hizo, mahakama
inatupilia mbali kesi hiyo kwa sababu waliofungua kesi, LHRC na TLS
hawakustahili kisheria kufungua kesi hiyo kwa sababu hawakuathirika.
0 comments:
Chapisha Maoni