Ijumaa, Juni 06, 2014

MATAPELI WAMFANYA KAZI MBWANA SAMATTA

MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na Klabu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta amewajia juu watu wanaotumia jina lake kufanya utapeli kupitia Mtandao wa Kijamii wa Facebook.
Samatta ambaye ameonyeshwa kukerwa kwa kiasi kikubwa na hali hiyo, amefikia uamuzi wa kutoa angalizo hilo baada ya kuwepo kwa taarifa za watu kutoa mikopo kwa kutumia jina lake.

Hivi karibuni kupitia akaunti inayosomeka kwa jina la Mbwana Aly Samatta, kulitolewa taarifa kuwa Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi amekabidhi msaada wa fedha kwa Taasisi ya Utoaji Mikopo Vicoba Tanzania ili kusaidia upatikanaji wa mikopo kwa kila Mtanzania atakayejiunga na taasisi hiyo.
Akizungumza moja kwa moja kutoka nchini DR Congo ambapo ndipo ilipo klabu yake, Samatta alisema hajawahi kuwa na akaunti yenye jina hilo na kudai kuwa iwapo kuna mtu au watu wanatumia jina hilo basi waache mara moja kwa kuwa linamchafua.
Mimi akaunti yangu inasomeka Mbwana Samatta ambayo ndiyo ninaitumia kwenye Facebook na kama kuna wengine wanatumia jina hilo, basi ni matapeli tu, kwani lengo lao ni kunichafua na kuniharibia.
Tabia kama hiyo kwa watu hao siyo nzuri hata kidogo kwa sababu mtu anaweza akafanya vitu vizuri au vibaya lakini watu wakajua ni mimi, naweza kuchukiwa na watu huku jambo likiwa limefanywa na mwingine.
Ninawaomba waache mara moja kwani siyo kitu kizuri, mimi ndiye nitakayepata matatizo kutokana na jina linalotumika. Naamini watu wanaotumia jina langu kwenye Facebook wapo wengi na wanafanya nishindwe kuwasiliana na mashabiki wangu
alisema Samatta.

0 comments:

Chapisha Maoni