Jumamosi, Juni 14, 2014

MWANAFUNZI WA DARASA LA KWANZA ALISHWA KINYESI

MWANAFUNZI wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Nyakabale wilayani hapa (jina limehifadhiwa), ameamrishwa kula kinyesi chake baada ya kukutwa akijisaidia kwenye kisima cha maji.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo, alisema jana kuwa mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Marco Maiko, alimwamuru mwanafunzi huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka nane, kula kinyesi hicho alichokuwa amejisaidia karibu na kisima chake.
Kamanda Konyo alisema mwanafunzi huyo akiwa na wenzake watatu, alijisaidia karibu na kisima hicho, na Maiko alimwamuru mwanafunzi huyo akile hadi kiishe na kwa hofu ya kupigwa alitii na kukila kinyesi hicho huku wenzake wakishuhudia.
Kamanda Konyo alisema baada ya kufika nyumbani, mwanafunzi huyo alimwambia mama yake, Agnes Lujaja (26), juu ya kilichotokea, ndipo mtuhumiwa alipokamatwa.
Alisema uchunguzi unaendelea, na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa mashitaka ya kudhuru mwili. Mwanafunzi huyo alipelekwa katika zahanati ya Nyakabale kwa matibabu zaidi.

0 comments:

Chapisha Maoni