MAHAKAMA ya Afrika inayoshughulikia masuala ya haki za binadamu, jana
imetoa hukumu katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher
Mtikila, ambayo italazimisha kusitishwa kwa Bunge la Katiba ili kupisha
utekelezaji wa sehemu ya hukumu hiyo ambayo ni ya kikatiba.
Katika hukumu hiyo, mahakama imeitaka serikali kutekeleza kwa vitendo
hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Juni 14, mwaka jana katika kesi ya
kudai mgombea binafsi katika uchaguzi wa ngazi zote, iliyofunguliwa na
Mchungaji Mtikila dhidi ya serikali.
Akisoma hukumu hiyo, Rais wa majaji wa mahakama hiyo, Jaji Sophia
Akuffor, mbele ya wawakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitaka
serikali ndani ya miezi sita kwanza kutangaza katika gazeti la serikali
hukumu iliyompa ushindi Mchungaji Mtikila ya mgombea binafsi na pia
kutangaza hukumu hiyo katika wavuti ya serikali.
Jaji huyo aliitaka serikali kuwasilisha katika mahakama hiyo
utekelezaji wa hukumu hiyo na kubainisha kuwa imeweka katika mchakato
suala la mgombea binafsi ili kutekeleza hukumu hiyo.
Alisema pia katika matangazo hayo, hukumu hiyo iwe imetafsiriwa
katika lugha nyepesi ya Kiswahili na Kiingereza ili kuwawezesha wananchi
wote kuisoma vizuri.
0 comments:
Chapisha Maoni