BABU aliyefunga ndoa mwaka 2011 akiwa na umri wa miaka 94, Mathias
Kisokota mkazi wa Kitongoji cha Isunta, Namanyere wilayani Nkasi ambaye
kwa sasa ana umri wa miaka 97, amehamia na mkewe katika Mji wa Mpulungu
mwambao wa Ziwa Tanganyika nchi jirani ya Zambia miezi sita iliyopita
kwa lengo la kufanya tambiko la kumwezesha mkewe mwenye umri wa miaka 83
kupata mtoto wa uzeeni.
Mke wa mzee huyo, Uria Mwamanzi ni mwenyeji wa nchi jirani ya Zambia
alizaliwa na kukulia katika Mji wa Mpulungu mwambao mwa Ziwa Tanganyika
ambapo kwa mujibu wa wajukuu zao ndiko babu yao alipokutana naye na kuwa
na mahusiano hadi walipofunga ndoa miaka mitatu iliyopita.
Wanandoa hao ambao waliacha gumzo kubwa baada ya kufunga pingu za
maisha katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Anthony, alasiri ya Juni 18,
2011 mjini Namanyere Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi.
Akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka katika Mji
wa Namanyere jana, Salvatory Adolf (19), mjukuu wa wazee hao kutoka kwa
mtoto wao kitindamimba mwenye umri wa miaka 40 sasa, alisema babu yake
amemsindikiza mkewe huyo ili kwenda kutambikia mizimu ya kwao.
Bibi hakuwa na raha mara kwa mara alikuwa akitamani kurudi nchini kwao Zambia kuwasalimia nduguze pia akiwa huku alikuwa akiugua mara kwa mara hivyo babu aliona bora amsindikize bibi akatambike kwa mizimu ya babu zake nchini humo
alisema.
Hata hivyo, hakutaka kueleza kwa undani juu ya kiu ya babu yake ya
kutaka kupata mtoto, habari ambazo zinazungumzwa na watu wa karibu
waliopo ndani ya familia ya wanandoa hao.
Miongoni mwao, Agnes ambaye ni mtoto wa mwisho wa Mzee Kisokota
akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka mjini
Namanyere, Nkasi alisema baba yake amekuwa na hamu hadi sasa ya kupata
mtoto katika ndoa yake changa.
Anasali sana akiomba kila siku apate mtoto katika ndoa yake.Bado ana matumaini makubwa ….. nikianza kukusimulia tutakesha, tena anasema siku akijaliwa mtoto katika ndoa yake hiyo atajawa na furaha kubwa na kufanya sherehe ya aina yake… amemsindikiza bibi (mkewe) Zambia kusalimia ndugu zake pia kutambika kwa kuwa baba ana hamu ya mtoto atatumia fursa hii nae kutambikia kwa wakwe zake ili mkewe huyo ashike mimba
alieleza Agnes.
Hali hiyo inakuja licha ya ukweli kwamba, umri wa mke wa Mzee
Kisokoto kuzaa umeshapitiliza, lakini kwa pamoja wamedaiwa kuamini kwa
Mungu hakuna kisichowezekana hivyo anaweza kutenda miujiza kwa kuwapa
baraka ya mtoto wa ndoa yao ya uzeeni.
Mjukuu huyo alipoulizwa juu ya ziara hiyo kuhusisha pia kusaka mtoto
kutoka kwa `mizimu’ ya ukoo wa mke wa babu yake, hakuwa na majibu ya
moja kwa moja.
Bibi alipoondoka alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mwili lakini tangu atambike nchini Zambia inadaiwa amepona kabisa na sasa wanaishi raha mustarehe na babu… ila watarudi huku kwetu baadae mwaka huu
alisema.
Katika safari ya wazee hao, Adolf anasema bibi na babu yake
walisindikizwa na Claudio Mathias (21), kaka wa mjukuu huyo na kwamba
kaka huyo amesharejea nchini.
Wanandoa hao kwa mujibu wa wajukuu zao kabla ya kufunga ndoa katika
Kanisa Katoliki Jimbo la Sumbawanga mjini Namanyere miaka mitatu
iliyopita walikuwa wakiishi ‘kinyumba’ kila mmoja wao akibahatika kuwa
na watoto katika mahusiano yake ya awali.
Kwa pamoja wana wajukuu zaidi ya 30 na vitukuu zaidi ya 40 wengi wao
wakiishi nchi jirani ya Zambia. Mzee Kisokoto alifiwa na mke wa kwanza
zaidi ya miaka 39 iliyopita.
0 comments:
Chapisha Maoni