TUKIO la mtoto Nasra Mvungi kuteswa kwa kufungiwa katika boksi ndani
ya nyumba kwa zaidi ya miaka mitatu na kufariki dunia baada ya kuokolewa
na wasamaria, limefanikisha kupatikana kwa mtoto mwingine mwenye
matatizo ya kiafya ambaye licha ya kuzaliwa miaka 18 iliyopita,
inaelezwa hajawahi kulia, kuongea, kukaa wala kutembea.
Mtoto huyo mwenye mwonekano kama wa mtoto mwenye umri wa miaka
mitano, amepatikana baada ya wasamaria kutoa taarifa Dawati la Jinsia
katika Jeshi la Polisi wilayani hapa, wakiarifu kuwapo kwa mtoto mlemavu
anayenyanyaswa kama ilivyokuwa kwa mtoto Nasra `Mtoto wa Boksi’.
Katibu wa Dawati la Jinsia, Koplo Janeth Maeda amethibitisha kuwapo
kwa tukio hilo, akisema walipokea taarifa za kuwapo kwa mtoto
anayenyanyaswa, hivyo kukimbilia eneo la tukio ili kumwokoa mtoto
aliyedaiwa kuwapo katika mateso ikiwa pamoja na kunyimwa huduma muhimu.
Hata hivyo, anasema walichokishuhudia si mateso, bali ni hali duni ya
kimaisha ya wazazi wake, hivyo kulilazimu Jeshi la Polisi kwa
kushirikiana na Ustawi wa Jamii kumwokoa kwa kumkimbiza hospitali kwa
uchunguzi zaidi wa afya yake.
Anasema:
Kwa kweli tulipopata taarifa hizo tulishtuka sana tukaamua kuwasha gari na kuelekea eneo la Lukobe ambako ndiko tuliambiwa kuwa kuna mtoto huyo na kumkuta mtoto huyo, lakini tofauti na tulivyoambiwa, tulimkuta akiwa katika mazingira mazuri.
Labda kilichoonekana kwa wengine kama ni mateso ni kwa sababu wazazi wake kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu tumeamua kusaidiana na ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa kumsaidia mtoto huyo kwa kuhakikisha anapatiwa huduma ya matibabu anayostahili.
Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo wa kike aitwaye Farida, baba
Abdallah Kipingu na mkewe, Mwajuma Abdallah, wakazi wa Lukobe katika
Manispaa ya Morogoro, binti yao huyo alizaliwa mwaka 1996 na kwamba
tangu azaliwe hajawahi kulia.
Mama wa mtoto, Mwajuma akiwa sambamba na mumewe alisema walimzaa
Farida huko Muheza mkoani Tanga na kwamba walimzalia nyumbani, lakini
kutokana na kushindwa kulia, wiki moja baadaye walikwenda Hospitali ya
Wilaya ya Muheza ili kujua kilichomsibu mtoto wao.
Hatukupata msaada, tukaendelea kumlea alipofikisha miezi minne ambao mara nyingi ni muda wa kukaa, tulijaribisha kumkalisha, lakini hakukaa hivyo kwa mara nyingine tukaenda hospitali, safari hii ya Mkoa wa Morogoro ambako tumekuwa tunaishi, tukaambiwa mtoto ahudhurie mazoezi ya viungo.
Tulihudhuria mazoezi kwa muda mrefu hatukuona mabadiliko baadaye tukaamua kuhamia kwenye kituo cha kulea watoto walemavu cha Amani Center, tukaambiwa tuendelee ingawa hakukuwa na mabadiliko, tulipohamia Lukobe mwaka jana hatukuweza tena kumpeleka kwenye mazoezi kutokana na kukosa uwezo wa kifedha za kufanya mizunguko
anasema.
Anasema wamekuwa wakiendesha maisha kwa kutegemea biashara ya bidhaa
ndogondogo katika genge lao, msimamizi mkuu akiwa mumewe na kwamba yeye
huhangaika zaidi na mtoto.
Hayo ndiyo yamekuwa maisha yetu hadi kufikia wakati huu tulipopata msaada wa Polisi na Ustawi wa Jamii
anasema mama huyo aliyeiomba jamii
kuwaombea na kuwapa msaada wa hali na mali katika kufanikisha matibabu
na malezi ya binti yao ambaye kwa sasa amefikishwa katika Hospitali ya
Mkoa wa Morogoro kwa uchunguzi zaidi.
Naye Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro, Oswin Ngungamtitu
aliwashukuru wananchi kwa kuitikia mwito wa kutoa taarifa za matukio
kama ya mtoto Nasra, kwani imewafanya wafumbue macho na kutoa taarifa
mbalimbali.
Alisema taarifa zao zinaweza kuwa faraja kwa watoto na wazazi wengi
wasiojua cha kufanya baada ya kuelemewa na majukumu ya kutunza watoto
wenye uhitaji maalumu.
Hata hivyo, aliitaka jamii kuwapeleka watoto wenye ulemavu na wenye
matatizo katika sehemu zinazohusika ili watoto hao waweze kupatiwa
msaada na hatimaye kuweza kuimarisha afya zao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk
Rita Lyamuya alisema baada ya kupata taarifa hizo taratibu za kumfanyia
uchunguzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na kumpatia virutubisho.
0 comments:
Chapisha Maoni