Serikali ya Kenya imepiga marufuku mikutano yote ya hadhara na kisiasa kwa muda usiojulikana katika mji mkuu Nairobi.
Inspekta mkuu wa polisi David Kimaiyo amesema
kuwa sababu ya kuharamishwa mikutano ya hadhara ni kuwa magaidi
wamepanga kufanya mashambulizi wakati wa mikutano yenyewe.
Akiongea baada ya mkutano wa maafisa
wote wa ulinzi mjini Nairobi, Kimaiyo amesema kuwa hawataruhusu
mikutano yoyote ya kisiasa wiki hii isipokuwa sherehe za kitaifa za
kuadhimisha miaka hamsini na moja tangu kenya kujinyakulia utawala wa
ndani kutoka kwa serikali ya Mkoloni.
Hizi zitakuwa sherehe za kusherehekea madaraka dei, zitakazofanyika tarehe mosi mwezi ujao.
Hata hivyo wakosoaji wa serikali wanasema kuwa
uamuzi huo, unalenga mkutano wa upinzani uliopangwa kufanyika mwishoni
wa wiki hii, kumlaki kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani CORD
ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ambaye amekuwa katika
ziara ya miezi miwili nchini Marekani.
Naibu spika wa bunge wa zamani, na mwanasiasa wa
upinzani Farah Maalim Mohamed amesema kuwa agizo hilo la inspekta mkuu
wa polisi, halina msingi wowote na linakiuka katiba ya Kenya.
Marufuku hii inakuja siku chache kabla ya mkutano wa hadhara wa kisiasa uliopangwa na muungano wa upinzani wa CORD
Muungano huo umesema kuwa mkutano wao utafanyika
kama ulivyopangwa, wakitaja marufuku hiyo kama ishara ya uoga kwa
upande wa serikali.
Akihutubia wandishi wa habari baada ya kauli ya
serikali kuharamisha mikutano, mmoja wa vigogo wa upinzani James Orengo,
alisema kuwa marufuku hiyo ni njama ya serikali kuanzisha mfumo wa
kidikteta sawa na uliokuwepo mapema miaka ya tisini.
Kiongozi mwingine wa upinzani Farah Maalim
alisema kuwa watafanya mkutano wao wa kisiasa Jumamosi licha ya agizo
hilo la serikali.
0 comments:
Chapisha Maoni