Jumamosi, Machi 25, 2017

MPANGO WA SAMATTA KUCHEZA SOKA UINGEREZA NA MAISHA YAKE AKIWA TANZANIA

Mcheza soka wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, amesema anapenda kucheza soka katika Ligi Kuu England ambako anavutiwa na uchezaji wa kiungo wa Chelsea, Eden Hazard.
Samatta ambaye kwa sasa anakitumikia kikosi cha KRC Genk cha Ubelgiji, hivi karibuni amekuwa na kiwango cha hali ya juu kilichozifanya timu nyingi za Ulaya kumtolea macho.
Hivi karibuni baba wa straika huyo, Ally Pazi Samatta, alisema mwanaye huyo angependa kwenda kucheza England kwa kuwa ndiyo ndoto yake ya muda mrefu kucheza huko.
Samatta alisema ni mapema mno kusema timu gani zinazomuwania kwa sasa, bali lengo lake siku moja kwenda kucheza soka England.
“Malengo yangu siku moja ni kwenda kucheza soka katika Nchi ya England japo kwa sasa timu nyingi zimeonyesha nia ya kunihitaji. Zipo timu za ndani na nje ya Ubelgiji, inavyoonekana zinasubiri mpaka kipindi kijacho cha usajili kifike ili waanze mchakato huo.
“Zamani nilivyokuwa mdogo, nilikuwa navutiwa na uchezaji wa Mussa Hassan Mgosi ambaye ndiye aliyenifanya mpaka leo hii kuwa mshambuliaji mahiri, lakini hivi sasa navutiwa na uchezaji wa Eden Hazard,” alisema Samatta.
Samatta leo Jumamosi ataiongoza Taifa Stars kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Vipi maisha yake akija Tanzania?
WADAU na mashabiki wengi wa soka huwa wanajiuliza swali hili kuwa straika Mbwana
Samatta anapokuja nchini kupumzika huwa anaishi wapi, Mbagala nyumbani kwao au sehemu nyingine kama wanavyofanya mastaa wa Ulaya.
Samatta ambaye ni straika ghali anayekipiga na Genk ya Ubelgiji, imebainika kwamba hufikia kwenye mjengo mmoja wa maana aliopanga (Apartment) maeneo ya Mtoni Kijichi.
Nyumba hiyo ipo ufukweni kabisa mwa bahari ya Hindi na inasemekana ndipo anapoishi binti aliyezaa naye mtoto wa kiume anayeitwa, Babually.
Rafiki yake wa karibu, alisema mpango huo ni wa siri na ngumu kuufahamu kwa sababu ya usalama na mambo mengine ya kiusumbufu yanayoweza kumpata staa huyo na hata familia yake haipendi ishu hiyo ijulikane.
“Anapokuja kwa mapumziko kwao huwa anakwenda kwa sababu ni nyumbani kwa ajili ya kusalimia na mambo mengine lakini hakai hapo, anaishi Kijichi kuna nyumba nzuri ya kifahari ipo ufukweni mwa bahari amepanga,”alisema.
“Kama ni majukumu ya timu anakaa na wenzake na Kijichi anakwenda mara moja kusalimia na anafanya hivyo kwa ajili ya usalama na mambo mengine kwa sababu anazo nyumba nzuri lakini hataki kwenda kukaa huko,”alisema na kufafanua maisha hayo ni kutokana na ushauri kutoka kwa watu wake wa karibu kutokana na
nafasi aliyonayo, sasa ni staa na hivyo anatakiwa kuishi kivingine.
Lakini meneja wa Samatta, Jamal Kasongo alikazia, Samatta anaishi Mbagala: “Samatta anaishi Mbagala, Mbagala ndiyo kwao, hawezi kuhama.”
Mwandishi alimtafuta, Samatta lakini ilikuwa ngumu kumpata lakini awali aliwahi kufika nyumbani kwao Mbagala anapoishi baba yake Mzee Samatta ambaye alionyesha chumba chake alichokitumia tangu alipokuwa mdogo hakikuwa na dalili ya kuishi staa huyo.
Samatta anazo nyumba tofauti kama tano zote ziko Mbagala katika maeneo tofauti kubwa anayoandaa kuishi mwenyewe hapo baadaye ipo Kibada imeisha, na marekebisho yanayofanyika ni madogo, Majimatitu, Kiburugwa Shimo la Mchanga, Mbande na Mbagala Saku lakini haishi huko.

0 comments:

Chapisha Maoni