Jumatano, Machi 29, 2017

MKOA WA RUVUMA NA MKAKATI MPYA WA KUPAMBANA NA MALARIA

MKOA wa Ruvuma kupitia mradi wa USAID Boresha Afya umelenga kuweka mikakati ya kumaliza ugonjwa wa malaria ambao ni mkubwa katika mkoa huo, ikilinganisha na kiwango cha kitaifa, hatua itakayowezesha kupungua kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge alisema kulingana na takwimu za kitaifa, katika mkoa wa Ruvuma wajawazito wanaopata kinga ya kwanza dhidi ya malaria (IPTp-1) ni asilimia 40 na inazidi kupungua hadi kufikia asilimia saba kwa wanaopata dozi ya kinga ya tatu (IPTp-3).
Dk Mahenge alitoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha kutambulisha Mradi wa USAID Boresha Afya kwa mkoa wa Ruvuma kilichofanyika katika Manispaa ya Songea.
Kwa mujibu wake, hata kiwango cha malaria kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ni asilimia 23 ilhali kitaifa ni asilimia 14 huku asilimia 39 ya kaya katika mkoa huo zinamiliki angalau chandarua kimoja na takwimu za kitaifa ni asilimia 54 na kuufanya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha chini nchini.
Alisema uzinduaji wa mpango huo ni faraja kubwa kwa serikali ya mkoa na wananchi kwa kuwa umelenga kutoa huduma shirikishi na endelevu kwa kufanya kazi na timu ya uendelezaji na usimamizi wa huduma za afya ya mkoa, halmashauri za wilaya na miji pamoja na asasi za kiraia zinazotekeleza afua za afya ngazi za jamii.
Dk Mahenge alivitaja vipaumbele vitakavyotekelezwa kuwa ni uhamasishaji jamii juu ya matumizi bora ya vyandarua, kinga ya malaria kwa wajawazito, kuzijua dalili za homa ya malaria na kuwahi kupata huduma katika vituo vya afya, sambamba na namna ya kuwakinga wajawazito kwa dawa za SP.
Aidha, vipaumbele vingine katika mradi huo ni kuboresha huduma za upimaji na utoaji wa huduma sahihi za tiba dhidi ya malaria kwa kufuata miongozo ya kitaifa na kuhakikisha upatikanaji wa dawa mseto (ACTS) pamoja na vitendanishi na hadubini.

0 comments:

Chapisha Maoni