Ivanka Trump amejiunga rasmi na
serikali ya babake ambapo atahudumu kama mfanyakazi asiyelipwa, kwa
mujibu wa ikulu ya White House.
Cheo chake halisi kitakuwa Msaidizi wa Rais.
Binti
huyo wa rais wa Marekani amekubali shinikizo baada ya wataalamu kuhusu
maadili kukosoa mpango wake wa awali wa kutaka kuhudumu katika wadhifa
usio rasmi.
Bi Trump, 35, amesema amesikia "maswali ambayo baadhi
ya watu wamekuwa wakiuliza kuhusu hatua yangu kumshauri rais katika
nafasi yangu kama mtu binafsi".
Mumewe, Jared Kushner, ni mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump.
Kupitia
taarifa, White House imesema ina furaha kwamba "Ivanka Trump amechukua
hatua hii isiyotarajiwa katika nafasi yake kama binti wa rais".
Bi Trump alisema kupitia taarifa yake kwamba amekuwa
akifanya kazi "kwa nia jema na kundi la washauri wa rais White House
pamoja na mshauri wake binafsi kujadili kuhusu jukumu lake".
Wataalamu
kuhusu maadili walilalamika ilipobainika wiki iliyopita kwamba Bi Trump
angepewa afisi White House pamoja na kibali cha usalama cha kuingia na
kuondoka ikulu hiyo, bila yeye kujiunga rasmi na wahudumu wa rais.
Wakosoaji walisema kazi ya Bi Trump inafaa kufanywa rasmi ndipo
aweze kudhibitiwa na sheria kuhusu uwazi wa maafisa wa serikali pamoja
na maadili. Aidha, adhibitiwe na sheria kuhusu mgongano wa maslahi.
Wakili
wa Bi Trump, Jamie Gorelick, amesema mteja wake atawasilisha nyaraka
zifaazo za kufichua utajiri wake kwa mujibu wa sheria kuhusu maadili ya
watumishi wa umma Marekani.
0 comments:
Chapisha Maoni