Ijumaa, Machi 31, 2017

CHUKI DHIDI YA UISLAMU AUSTRIA YAONGEZEKA KWA 62%

Kumeshuhudiwa ongezeko la 62% la chuki dhidi ya Uislamu nchini Austria mwaka 2016.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Ushauri kwa Waislamu Austria, idadi ya hujuma za chuki dhidi ya Waislamu zilifika 253 mwaka 2016 ikilinganishwa na 156 mwaka 2015.
Uchunguzi umebaini kuwa aghalabu ya waliolengwa ni wanawake Waislamu ambao wengi wao walihujumiwa wakiwa katika usafiri wa umma au maeneo mengine ya umma. Kwa kawaida wanawake Waislamu hulengwa kwa sababu ni rahisi kubaini dini yao kutokana na uvaaji wao wa vazi la staha la  Hijabu.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa asilimia 31 ya hujuma zilikuwa kwa njia ya maandishi au matamshi huku asilimia 30 nyingine ikiwa ni katika fremu ya hotuba zilizojaa chuki. Aidha asilimia 12 ya hujuma hizo zililenga taasisi za Kiislamu na asilimia tano zilikuwa ni kuhujumiwa kimwili.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa baadhi  ya hujuma dhidi ya Waislamu zilijiri ndani ya taasisi za kiserikali nchini Austria.
Kituo cha  Ushauri kwa Waislamu Austria kilianzishwa mwaka 1979 na kilianza kusajili hujuma dhidi ya Waislamu mwaka 2014. Kituo hicho kinatoa ushauri nasaha kwa Waislamu walioathirika na hujuma za wenye chuki dhidi ya Uislamu.
Kati ya watu milioni tisa nchini Austria, takribani 600,000 ni Waislamu, wengi wakiwa ni wenye asili ya Uturuki.
Mwezi Januari serikali ya Austria ilitangaza kuwa wafanyakazi wote wa umma nchini humo, wakiwemo walimu, watapigwa marufuku kuvaa Hijabu wakiwa kazini.
Sheria ya kupiga marufuku vazi la staha la Kiislamu, Hijabu inatayarishwa na Sebastian Kurs, Waziri wa Mambo ya Nje wa Austria ambaye pia anashughulikia masuala ya namna wahajiri wa kigeni wanavyopaswa kufuata utamaduni wa nchi hiyo.

0 comments:

Chapisha Maoni