Ijumaa, Machi 31, 2017

MAHAKAMA YA KENYA YASIMAMISHA MPANGO WA MADAKTARI WA TANZANIA KUAJIRIWA NCHINI HUMO

Mahakama ya Leba nchini Kenya imesimamisha mpango wa serikali wa kuwaajiri mamia ya madaktari kutoka nchi jirani ya Tanzania.
Hakimu Nelson Abuodha wa Mahakama ya Ajira na Uhusiano wa Kikazi nchini Kenya ametoa uamuzi huo kufuatia ombi la madaktari wa Kenya wanaopinga utekelezwaji wa mpango huo. 
Madaktari hao wanasema kuna idadi kubwa ya madaktari waliohitimu nchini Kenya ilhali hawana ajira, na hivyo hawaelewi kwa nini serikali inataka kuleta madaktari kutoka nje ya nchi. Aidha wameitaka mahakama iishurutishe serikali kuwaajiri madaktari 1,400 wa Kenya ambao wamehitimu na hawana ajira.
Rais John Magufuli wa Tanzania aliidhinisha utekelezaji wa ombi la serikali ya Kenya la kupatiwa madaktari 500, baada ya kukutana na Waziri wa Afya wa nchi hiyo Cleopas Mailu mjini Dar es Salaam Machi 18.
Itakumbukwa kuwa, serikali ya Kenya ilichukua uamuzi huo kufuatia mgomo wa madaktari wa nchi hiyo katika hospitali za umma uliodumu kwa siku 100, kulalamikia mishahara duni na mazingira magumu ya kazi.
Hata hivyo Wizara ya Afya, Baraza la Magavana na Muungano wa Madaktari nchini humo KMPDU baada ya mashauriano marefu na vikao vya faragha walifikia makubaliano yaliyosainiwa mapema mwezi huu na kuhitimisha mgomo huo, ambao ulitikisa sekta ya afya nchini Kenya.

0 comments:

Chapisha Maoni