Taasisi moja ya kuwahami watoto wa Kiafrika imetangaza kuwa, katika uchaguzi wa hivi karibuni nchini Uganda watoto sita waliuawa au kukatwa viungo kwa imani za kishirikina.
Taasisi hiyo inayojulikana kwa jina la Kyampisi Childcare Ministries (KCM) imetangaza kuwa, wagombea wa uchaguzi wamekuwa wakiwakata viungo au kuwaua watoto kwa imani za kishirikina wakiamini kwamba, kufanya hivyo kutawafanya wapate mafanikio katika nyadhifa wanazogombea. Ripoti ya asasi hiyo inaelezwa kuwa, ni ada ya kale nchini Uganda inapowadia kipindi cha uchaguzi watoto hukatwa viungo au kuuawa kwa imani za kishirikina. Wagombea wa nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi hufanya hivyo wakidai kwamba, wanawatoa kafara watoto wao ili mambo yawanyokee katika uchaguzi. Shelin Kasozi mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo ya Kyampisi Childcare Ministries (KCM) amesema, baadhi ya wahusika wanaamini kwamba, kumwagwa damu huleta mafanikio na madaraka. Taarifa zaidi zinasema kuwa, Oktoba mwaka jana hadi Februari mwaka huu kuliripotiwa kesi za kukatwa viungo watoto au kuuawa kwa imani hizo za kishirikina katika Wilaya za Ssembabule, Mukono, Buikwe na Mubende katikati mwa Uganda.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, Yoweri Museveni alishinda tena kiti cha Urais baada ya kupata zaidi ya asilimia 60 ya kura huku mpinzani wake mkuu, Kizza Besigye akipata asilimia 35.4.
Wapinzani wakuu nchini Uganda wameyakataa matokeo ya uchaguzi huo wakisema hayakuakisi uhalisia wa mambo katika zoezi la upigaji kura.
0 comments:
Chapisha Maoni