Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetangaza kuiunga mkono Polisi nchini katika operesheni ya kukamata wateja wa makahaba kuhakikisha biashara hiyo inakoma nchini.
Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu alisema takwimu zinaonesha wanawake ndio waathirika wakubwa wa ugonjwa wa Ukimwi, ambapo kati ya Watanzania 10 wanaopimwa, sita ni wanawake na wanaume ni wanne pekee.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Dar es Salaam jana, Ummy alisema si haki kuwakamata wanawake wanaojiuza na kuwaacha wateja wao ambao ni wanaume.
“Ninalipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo kwa sababu imeonesha kutoegemea upande mmoja kwa kuwakamata wanawake makahaba. Wote wanaojiuza na wanaonunua huduma hiyo ni wakosaji wanaostahili kuchukuliwa hatua za kisheria.Tunaungana na Polisi kushiriki operesheni hiyo,” alisema.
Alieleza kuwa, biashara ya ukahaba inayofanywa na wanawake isingekuwepo endapo wateja wasingekuwepo, hivyo, wateja wanastahili kukamatwa pia kwa sababu ndio wanaoichochea.
Ummy alisema familia nyingi zina misukosuko na wanawake wengi wamekuwa wakiteseka na wengine kuambukizwa magonjwa na waume zao wanaoshiriki biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, alisema sasa wanataka kuona idadi ya wanaume wateja wa biashara hiyo inatajwa sambamba na ya wanawake wanaokamatwa nao ili ndugu na wake zao wafahamu kuhusu tabia yao hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, alisema hatua ya kukamata wateja na wauza miili imetokana na makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni