Alhamisi, Machi 10, 2016

WAANGALIZI KUTOSHIRIKI MARUDIO YA UCHAGUZI ZANZIBAR

Muungano wa Waangalizi wa Ndani wa Uchaguzi (Cemot) umesema hautashiriki katika uangalizi wa uchaguzi wa marudio Zanzibar utakaofanyika Machi 20 mwaka huu kutokana na kukabiliwa na ukata.
Cemot ni umoja wa taasisi za waangalizi wa ndani wa uchaguzi inayohusisha Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi (Temco) na Muungano wa taasisi zisizo za kiraia za kusimamia uchaguzi (Tacceo) ambazo zilitumia waangalizi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari Arusha katika warsha ya mrejesho wa taarifa ya waangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu, Mwenyekiti mwenza wa Cemot, Martina Kabisama alisema fedha zote zilitumika katika uchaguzi uliopita.
“Kwenda kuangalia uchaguzi ni jambo linalohitaji rasilimali, hivyo hatutakwenda Zanzibar katika uchaguzi wa marejeo kwa kuwa tulikuwa hatujaandaa andiko la kupata fedha za uchaguzi huo,” alisema.
Kabisama alisema Cemot ilikuwa na waangalizi wa muda mfupi 9,400 na wengine 350 waliotoka Tacceo na Temco.
Mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu kwa Tanzania Bara na Visiwani, Dk Alexander Makulilo alisema Cemot ilifanya kazi kubwa katika uangalizi na imeandaliwa taarifa inayoonyesha mahitaji ya maboresho katika chaguzi zijazo.
Dk Makulilo ambaye anaongoza timu ya uandishi wa taarifa ya Cemot, alisema uchaguzi wa Zanzibar uliopita ulikwenda vizuri licha ya kuwapo dosari kidogo sawa na Tanzania Bara.
Alisema Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na mashirika yasiyo ya kiserikali, walifanya kazi ya kutoa elimu ya wapigakura, tofauti na Tanzania Bara.
Pia alisema visiwani humo polisi walitekeleza vizuri wajibu wao tofauti na Tanzania Bara.
Dk Makulilo alisema asilimia 87 ya waangalizi wa Zanzibar walieleza polisi walifanya kazi nzuri kwa asilimia 65 kutokana na kusimamia vema uchaguzi.

0 comments:

Chapisha Maoni