Wagombea wanaowania kiti cha urais huko Uganda wako tayari kushiriki uchaguzi huo uliopangwa kufanyika kesho Alhamisi Februari 18, baada ya kumalizika muda wa kampeni za uchaguzi nchini humo.
Uchaguzi wa Rais na Bunge wa Uganda utafanyika kesho Alhamisi kote nchini humo kwa wakati mmoja kama ilivyopangwa. Katika uchaguzi huo wa kesho, Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo anachuana na wagombea wengine saba walioteuliwa na vyama vya upinzani kupeperusha bendera za vyama vyao katika kinyang'anyiro hicho wakiwemo wagombea binafsi.
Museveni ambaye amekuwa madarakani Uganda tangu mwaka 1986 ameshagombea mara saba katika chaguzi za rais nchini humo.
Museveni sawa kabisa na baadhi ya viongozi wa kizazi kikongwe cha Kiafrika, mwaka 2005 aliweza kuifanyia marekebisho katiba ya Uganda na hivyo kuandaa uwanja wa kusalia madarakani kwa miaka mingine kadhaa. Kwa mujibu wa Katiba ya Uganda mtu yoyoye anayetaka kugombea kiti cha urais anapasa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 75. Rais Yoweri Kaguta Museveni ambaye ana miaka 71 ataweza kusalia madarakani hadi mwisho wa duru ya urais yaani hadi miaka mitano ijayo, iwapo atashinda uchaguzi wa kesho. Museveni kama walivyofanya baadhi ya Marais wa nchi za Kiafrika kama wa Equatorial Guinea, Angola na Zimbabwe ni viongozi waliodumu kwa muda mrefu zaidi katika hatamu za uongozi ambao kwa mara ya kwanza waliingia madarakani katika miaka ya muongo wa 80.
Weledi wa masuala ya kijamii wanaona kuwa kusalia madarakani Yoweri Museveni katika nchi kama Uganda ambayo asilimia 78 ya jamii ya watu wa nchi hiyo wapatao milioni 38 inatokana na vijana walio na umri wa chini ya miaka 30, ni hatua ambayo itasababasha ufa kati ya vijana. Wagombea saba watakaochuana katika uchaguzi wa Rais wa Uganda hapo kesho, watano kati yao walishiriki katika vita vya msituni katika muongo wa 80 kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Yoweri Museveni alikuwa kiongozi wa Harakati ya Msituni ya Mapambano ya Taifa wakati wa vita vya ndani nchini Uganda, ambayo ilibadilishwa na kuwa chama cha kisiasa baada ya yeye kuingia madarakani mwaka 1986. Hii ni katika hali ambayo Daktari Kiiza Besigye ambaye ni mgombea wa kiti cha urais kutoka chama kikuu cha upinzani cha FDC , na Amama Mbabazi Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda ambao ni mahasimu wa Museveni katika uchaguzi wa Rais wa kesho, walipigana pamoja na kiongozi huyo katika vita vya msituni vya Uganda katika muongo wa 80.
Besigye ambaye ameshindwa na Museveni mara tatu mfululizo katika chaguzi zilizopita, amesema mbele ya umati wa wafuasi wake katika kampeni za uchaguzi hivi karibuni kuwa anatumai atashinda kwenye uchaguzi wa Rais wa kesho. Matamshi hayo yaliyozua makelele ya Daktari Kiiza Besigye yalisababisha kutiwa mbaroni na polisi yeye pamoja na baadhi ya wafuasi wake. Hata hivyo Kiiza Besigye muda mfupi baadaye aliachiwa huru. Besigye mgombea wa kiti cha urais wa chama kikuu cha upinzani nchini Uganda FDC chini ya nara ya "mabadiliko" ameazimia kushinda kura nyingi za wananchi khususan za tabaka la vijana.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa shaari ya "Mabadiliko" inayonadiwa na Besigye itavutia na kuzingatiwa pakubwa na kizazi cha vijana wa Uganda ambao kwa miongo mitatu mtawalia wameshuhudia Uganda ikiongozwa na Museveni chini ya chama tawala cha NRM.
Katika upande wa pili Amama Mbabazi Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda ambaye ni mmoja wa waasisi wa chama tawala NRM, huko nyuma alikuwa akihesabiwa kuwa katika waitifaki wa Museveni, hata hivyo alimua kuondoka chama tawala baada ya kuibuka vita vya kuwania madaraka kati yake na Museveni mwaka 2014. Hivi sasa baada ya chama cha Amama Mbabazi kujiunga na vyama vinne vya upinzani huko Uganda, kesho kitashiriki katika uchaguzi wa Rais kama chama kimoja baada ya kuasisiwa Muungano wa Kidemokrasia kati ya vyama hivyo.
Daktari Kiiza Besigye pia alijiondoa katika chama tawala cha NRM mwaka 2001 na kujaribu pakubwa kuhitimisha uongozi wa Museveni huko Uganda kwa kushiriki mara kadhaa katika uchaguzi wa rais nchini. Besigye tayari amedai kuwa uchaguzi wa kesho utakuwa si wa kiadilifu na usio wa wazi. Amesema kuwa yeye na chama chake wataendelea kupigania utawala wa kidemokrasia huko Uganda. Tukitupia jicho siasa za Uganda tangu ipate uhuru wake hadi sasa, tunaona kuwa nchi hiyo haijawahi kukabidhi madaraka kwa amani. Iwapo Museveni atashinda uchaguzi wa rais wa mwaka huu pia, basi hii itakuwa ni mara ya mwisho kwa kiongozi huyo kuwa rais wa nchi kwa mujibu wa katiba mpya ya Uganda; japokuwa upo pia uwezekano kwa Museveni kusalia madarakani kama wafanyavyo watawala wengi wa nchi za Kiafrika kwa kuifanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo kwa mara nyingine tena.
0 comments:
Chapisha Maoni