Wananchi wa Uganda waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanaelekea katika vituo vya kupigia kura kumchagua Rais na wawakilishi wao wa Bunge.
Inaelezwa kuwa, raia wapatao milioni 15 wa nchi hiyo waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wanamchagua Rais mpya wa nchi hiyo pamoja na wawakilishi wao wa Bunge lijalo. Wagombea wanane wanachuana kuwani kiti cha Rais.
Hata hivyo kati ya wagombea hao wanane ni watatu tu miongoni mwao ndio waliotajwa sana katika kampeni za uchaguzi huo. Rais Yoweri Museveni ambaye amekuwa madarakani nchini Uganda tangu mwaka 1986 anachuana na Kizza Besigye mgombea wa chama cha FDC na Amama Mbabazi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wake.
Uchaguzi wa leo unafanyika huku wapihzani wakiendelea kulalamika kwamba, serikali ya Rais Museveni imekuwa ikiwabana na kuwakandamiza wafuasi wao hasa katika kampeni za uchaguzi wa mara hii.
Huku Tume ya Uchaguzi ya Uganda ikisisitiza kwamba, uchaguzi wa leo utakuwa huru na wa haki, wagombea wa upinzani wameonya kuhusiana na hatua yoyote ile ya kuiba kura au kufanya udanganyifu.
Amama Mbabazi amesema, hatayakubali matokeo ya uchaguzi huo endapo itabainika kwamba, kulikuwa na mchezo mchafu wa kuiba kura.
Weledi wa mambo wanasema, kuna uwezekano mkubwa Rais Museveni akashinda tea kiti cha urais na kuendelea kutawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
0 comments:
Chapisha Maoni