Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema kuwa mgombea urasi wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump si Mkristo.
Matamshi hayo ya Papa Francis ni kielelezo cha wasiwasi unaoongezeka kimataifa kuhusu mielekeo na mitazamo ya bilionea huyo anayewania kiti cha Rais wa Marekani.
Papa Francis amewaambia waandishi habari nchini Mexico kwamba, mtu anayefikiria kujenga kuta za kutenganisha watu na si kujenga daraja la kuwaunganisha si Mkristo.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki ametoa matamshi hayo baada ya mwanasiasa huyo wa Marekani anayezusha mjadala mkubwa kimataifa kutokana na maoni na mitazamo yake ya ajabu na wakati mwingine ya kibaguzi kusema kwamba, iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani atajenga ukuta katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico ili kuzuia wahajiri kuingia Marekani.
Hivi karibuni pia Waingereza nusu milioni walisaini waraka unaoitaka serikali ya nchi hiyo kumzuia Donald Trump kuingia nchi humo baada ya kutoa wito wa kuzuiwa Waislamu kuingia Marekani. Vilevile alitoa wito wa kutumiwa mbinu za Manazi wa Ujerumani chini ya uongozi wa Adolph Hitler dhidi ya wafuasi wa dini hiyo ya Mwenyezi Mungu.
0 comments:
Chapisha Maoni