Alhamisi, Februari 18, 2016

MUSEVENI AONGOZA MATOKEO YA AWALI YA UCHAGUZI

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Uganda yanaonyesha kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama tawala cha NRM, Yoweri Kaguta Museveni anaongoza kwa kupata kura nyingi zaidi zilizohesabiwa.
Mkuu wa Time ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda, Badru Kiggundu ametangaza mapema leo kwamba Yoweri Museveni anaongoza kwa kupata asilimia 63.67 ya kura zilizokuwa zimehesabiwa hadi wakati wa kutolewa taarifa hiyo. Dr. Kizza Besigye anayewakilisha chama kikuu cha upinzani cha FDC alikuwa katika nafasi ya pili akiwa na asilimia 32.4 na waziri mkuu wa zamani Amama Mbabazi alikuwa katika nafasi ya tatu baada ya kupata asilimia 1.22 ya kura zilizokuwa zimehesabiwa.
Uchaguzi wa Rais na Bunge nchini Uganda ambao ulianza saa moja asubuhi jana ulimalizika saa moja jioni bila kuripotiwa visa vikubwa vya uhalifu. Hata hivyo kuliripotiwa machafuko katika baadhi ya vituo vya kupigia kura baada wananchi kulalamika dhidi ya kucheleweshwa karatasi za kupigia kura. Ripoti zinasema polisi ya Uganda ilitumia gesi za kutoa machozi kutawanya na kutuliza watu waliokuwa wakilalamika katika vituo hivyo.
Uchaguzi wa Rais na Bunge katika majimbo 38 ya uchaguzi nchini Uganda unatarajiwa kufanyika leo Ijumaa baada ya kujitokeza matatizo ya kufanyika zoezi hilo hiyo jana.
Serikali ya Uganda jana ilifunga mitandao ya kijamii kama facebook, twitter na Whatsapp ikisisitiza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa sababu za kiusalama.

0 comments:

Chapisha Maoni