WAFANYABIASHARA wa Rwanda wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Rais John Magufuli katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa kuimarisha ufanisi wa bandari, kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi jirani.
Aidha wamesema tangu Rais Magufuli aanze kuchukua hatua hizo, mizigo yao imekuwa salama zaidi na wamefanikiwa kuipata kwa urahisi tofauti na zamani ambapo mingi ilikuwa ikipotea.
Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza baada ya kutua nchini akitokea Kigali, Rwanda, Balozi Mahiga alisema pia Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame amemhakikishia kuwa ataendelea kushawishi wafanyabiashara wake kutumia Bandari ya Dar es Salaam, ili kukuza uhusiano wa kibiashara uliopo.
“Nilipata bahati ya kuzungumza na wafanyabiashara wa kule... wamepongeza sana hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli pale bandarini kwa sababu wanasema sasa hivi itawasaidia sana kuhakikisha usalama wa mizigo yao,” alisema Blozi Mahiga.
Alisema wafanyabiashara hao pia wameomba mkutano wa pamoja na wenzao wa Tanzania, ili kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo fursa za uwekezaji ndani ya Rwanda na Tanzania.
Alisema Rais Kagame anaunga mkono ujenzi wa reli itakayotumika kusafarisha mizigo kwa kuwa ni njia mojawapo ya kukuza uchumi wa nchi hizo mbili rafiki.
Akizungumzia safari yake hiyo, Balozi Mahiga alisema, alienda nchini humo kujadiliana masuala mbalimbali aliyoagizwa na Rais Magufuli kwa Rais wa nchi hiyo, ambapo walijadili masuala matatu, ikiwemo machafuko yanayoendelea Burundi.
Alisema kuhusu machafuko ya Burundi, Rais Kagame alikanusha tuhuma zinazotolewa na nchi hiyo pamoja na jumuiya za kimataifa kuwa anahusika katika kuchochea machafuko hayo.
Kwa mujibu wa Balozi Mahiga, maandamano ya nchi nzima yaliyofanyika wiki iliyopita nchini Burundi ya kuishutumu Rwanda kuhusika na machafuko nchini mwao, yalishitua nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na baadhi ya maneno ya chuki yaliyokuwa yakitolewa na wananchi hao dhidi ya nchi hiyo.
Alisema hali hiyo, ilihofiwa kwamba ingeweza kuvunja mazungumzo ya kutafuta suluhu yanayoendelea. “Nilimuuliza Rais Kagame kuhusu hili suala, akasema hatachukua hatua yoyote licha ya kwamba wananchi wake wamemlazimisha kufanya kitu. Lakini alisema atashiriki katika majadiliano ya kutafuta suluhu ya Burundi. “Sisi tulikuwa tunahofia kuwa huenda akachukua hatua ambazo zingeweza kuleta matatizo na hata mazungumzo yanayoendelea kuvunjika, lakini ameniambia hatachukua hatua yoyote inayoweza kusababisha kuvunjika kwa uhusiano,” alisema Balozi Mahiga.
Hata hivyo, alisema Rais Kagame alilalamikia nchi yake kushutumiwa kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wakimbizi wa Burundi, ili kuipindua Serikali ya nchi hiyo na kutaka Jumuiya za Kimataifa, kuwaondoa wakimbizi zaidi ya 70,000 na kuwahamishia nchi nyingine za jirani.
“Aliniambia kuwa kuendelea kuwa na hawa wakimbizi katika nchi yake, kunaweza kumletea matatizo makubwa, kwa sababu amekuwa akilaumiwa sana. Hivyo kuliko lawama, ni bora hizi Jumuiya za Kimataifa zikawaondoa wakimbizi,” alisema.
Alisema kwa mujibu wa Rais Kagame, Rwanda itaendelea kushiriki katika mijadala mbalimbali ya kutafuta suluhu ya Burundi na itahakikisha Burundi inakuwa salama.
Jambo lingine walilozungumza na Rais Kagame ni mkutano wa marais wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, unaotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi nchini Tanzania, ambapo pia alikuwa katika hatua ya mwisho katika kukamilisha ajenda na watakaoshiriki mkutano huo.
0 comments:
Chapisha Maoni