BAADA ya muda mrefu wananchi kufuata huduma za upasuaji kwa njia ya teknolojia mpya ya Vitundu nchini India, Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya imeanza kutoa huduma na hiyo kupunguza gharama kubwa za kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi.
Huduma hiyo ilizinduliwa juzi ambapo ilitanguliwa na semina pamoja na mafunzo kwa wataalamu juu ya namna ya kuvitumia vifaa ambavyo ni vipya kwao, na baadaye kufanya kwa vitendo kwa kufanya upasuaji wa wagonjwa Saba.
Madaktari Bingwa wa upasuaji katika Hospitali hiyo ya kanda ya Mbeya, waliungana na wataalamu kutoka Ujerumani ambao ndio walioleta neema hiyo ambayo inajulikana kama upasuaji kwa njia ya vitundu inayojulikana kwa jina la kitaalamu ‘Raparascopic Tower’
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Thomas Isdory, alisema kuwa huduma hiyo ya Upasuaji kwa kutumia teknolojia ya Vitundu, imeanzia kwa wananchi wote ambao ni wanachama wa Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya.
Amesema kuwa wameanza na wanachama wa mfuko huo kutokana na kwamba mfuko huo tayari ulishatoa gharama za matibabu kwa kutumia teknolojia hiyo na kwama utaratibu kwa wananchi wengine utaanza baadaye.
Isdory amesema kuwa changamoto kubwa inayoikabili Hospitali hiyo ni uhaba wa madaktari bingwa, ambapo amesema kuwa hospitali ina madaktari bingwa wa upasuaji wanne tu ambao hawatoshi kulingana na mahitaji.
Alifafanua kuwa kati ya madaktari bingwa hao wawili wapo katika kitengo cha upasuaji wa akina mama Meta huku wengine wawili wakiwa katika Hospitali kuu wakifanya upasuaji wa magonjwa ya kawaida.
“ Kwa kuanzia tumeanza na wagonjwa ambao ni wateja wa mfuko wa bima ya Afya kutokana na kwamba wenzetu wa Bima tayari walishatangaza bei za matibabu kwa kutumia teknolojia hii mpya, lakini taratibu zinaendelea kupanga bei kwa ajili ya watu wengine ili wote waweze kuipata,” alisema Isdory.
Dk. Guydon Makulila ambaye ni mtaalamu wa madawa ya usingizi alisema kuwa teknolojia hiyo ni nzuri kuliko ile ya kuchana kutokana na kwamba yenyewe mgonjwa hapati maumivu makali kutokana na kwamba vinatobolewa vitundu vidogo.
Amesema kuwa pia haina hatua nyingi kutokana na kwamba mgonjwa hukaa kwenye dawa kwa muda mfupi kabla ya kufanyiwa upasuaji huo na kwamba hakuna mgonjwa kurudi tena Hospitali kwa ajili ya kutoa nyuzi.
Alidai kuwa mgonjwa hupata nafuu haraka kuliko ile ya kuchana na kwamba mgonjwa hupana fahamu baada ya muda mfupi na kuweza kujieleza vizuri tofauti na ile ya zamani.
“Operasheni kwa kutumia teknolojia hii ni nzuri sana maana haina mgonjwa hapati maumivu makali sana kama ilivyo kwa ile ya kuchana, hakuna mgonjwa kukaa muda mrefu kwenye dawa, pia mgonjwa hupata nafuu haraka na hakuna kurudi ili kutolewa nyuzi,” alisema Dk. Makulila.
Nao baadhi ya wagonjwa waliokuwa wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia teknolojia hiyo akiwemo Edda Kayinga na Anna Edward ambao wote walitolewa mawe kwenye mfuko wa nyongo walisema kuwa huduma hiyo ni nzuri kutokana na kwamba inafanyika haraka na hata maumivu yanakuwa ya kawaida.
0 comments:
Chapisha Maoni