Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote kuwa makini
na wakuzaji Sanaa (Mapromota) au baadhi ya wanaojiita wadau wa Sanaa
ambao wamekuwa wakitumia njia za kiulaghai na utapeli katika kujipatia
faida na manufaa kupitia mgongo wa Wasanii.
Baraza linatoa angalizo hili
kufuatia kuwepo kwa ongezeko la matukio ya baadhi ya watu wanaojiita
wadau wa Sanaa ambao wamekuwa wakiwadanganya wasanii na kuwalaghai kwa
kuwaahidi fursa mbalimbali kama za maonesho ya ndani na nje ya nchi ambazo hata hivyo zimekuwa zikiishia katika kuwaletea wasanii matatizo kiuchumi na kijamii.
Aidha, watu hao wamekuwa wakitumia majina ya viongozi wa Serikali
kuwatapaeli wasanii na kujipatia fedha isivyo halali.BASATA linapenda
kuwakumbusha wasanii kwamba kabla hawajaingia makubaliano yoyote na mtu,
asasi au kampuni yoyote wawasiliane na wanasheria au watoe taarifa
Ofisi za Utamaduni za wilaya au manispaa zilizo karibu nao ili
kuhakikisha wanaepuka ulaghai na udanganyifu kutoka kwa watu hao wasio
waaminifu.
Aidha, kwa wasanii walioko Dar es Salaam BASATA
linawaelekeza kufika Ofisi zake zilizoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar
es Slaam ili wapate msaada wa kisheria na kujiridhisha kama makubaliano
yao ni halali na ya uhakika.
Mwisho kabisa, BASATA linapenda
kuwakumbusha wasanii kwa ujumla kwamba, tangu Januari Mosi mwaka 2013
tasbia za muziki na filamu ni rasmi hivyo Wasanii wote hawana budi
kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na wanafanya kazi kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu za uendeshaji wa kazi za Sanaa
nchini.
Aidha, kila msanii anawajibika kuhakikisha anafanya kazi
na mtu, watu, asasi au kampuni iliyo na vibali halali vya kuendesha
shughuli za Sanaa na si vinginevyo.
0 comments:
Chapisha Maoni