Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza
kuwa, watu wasiopungua 140 wameuawa wakati vikosi vya serikali ya
Ethiopia vilipokuwa vinakabiliana na malalamiko ya wapinzani wa
serikali.
Machafuko hayo yamezuka baada ya serikali kujaribu kuendeleza miradi
yake ya kuupanua mji mkuu kwenye eneo moja la kilimo. Watu wenye hasira
wa eneo hilo wakiwemo wanachuo, wamemiminika mitaani kulaani kitendo
hicho cha serikali ya Ethiopia na kusema kuwa ni kupora ardhi za watu
ambao njia pekee ya kuendeshea maisha yao ni kilimo.
Mashirika ya haki za binadamu yameripoti kuwa, machafuko hayo
yaliyoanza wiki kadhaa nyuma, yameshapelekea watu wasiopungua 140
kuuliwa na vikosi vya serikali katika eneo la Oromia.
Shirika la Human Rights Watch lilitangaza jana (Ijumaa) kuwa, huo ni
mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Ethiopia tangu ule wa
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005.
Kwa mujibu wa shirika hilo, watu wengine wengi wamejeruhiwa kwenye machafuko hayo.
Human Rights Watch limeongeza kuwa, idadi ya wahanga wa machafuko hayo ni kubwa sana.
Hadi tunapokea habari hii, serikali ya Ethiopia ilikuwa imedai ni
watu watano tu ndio waliouawa kwenye machafuko hayo hadi hivi sasa.
0 comments:
Chapisha Maoni