Jumanne, Januari 19, 2016

WATOTO MIL 2.6 HUFA KABLA YA KUZALIWA DUNIANI KOTE

Utafiti mpya wa tiba unasema watoto milioni mbili nukta sita wanafariki kabla ya kuzaliwa duniani kote kila mwaka, na theluthi mbili ya vifo hivyo vinatokea barani Afrika.
Akichapisha ripoti yake katika jarida la The Lancet, jopo la wataalamu kutoka chuo cha afya mjini London limesema kumekuwa na maendeleo finyu katika kupunguza idadi ya vifo vya watoto kabla ya kuzaliwa licha ya kuwa vinaweza kuepukika.
Miongoni mwa taarifa za kushangaza katika ripoti hiyo, ni kwamba itachukua zaidi ya miaka mia moja na sitini kwa mwanamke wa kawaida anaetoka katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara kuweza kujifungua mtoto aliyehai kama ilivyo kwa mwanamke katika nchi zenye pato la juu.
Katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara, utafiti huo unasema, asilimia sitini ya vifo vya watoto wanaozaliwa vinatokea katika maeneo ya vijijini.
Katika bara la Afrika, nchi ya Nigeria ndio inaongoza kwa idadi kubwa ya vifo hivyo, huku ikiwa na zaidi ya vifo mia tatu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ya ujauzito.
Miongoni mwa habari njema ni nchi ya Rwanda ambayo imeweza kubadilisha mwelekeo na kupunguza idadi ya vifo hivyo.
Waandishi wa ripoti hiyo wanasema, uboreshaji umefanyika zaidi katika afya ya kina mama na vifo vya watoto, lakini sio katika kupunguza vifo vya watoto ambao hawajazaliwa.
Wamesema, watoto hawapaswi kuzaliwa katika ukimya na wazazi wao hawapaswi kuomboleza kimya kimya.

0 comments:

Chapisha Maoni