Jumanne, Januari 19, 2016

WAMOROCCO WAANDAMANA KUPINGA MISHAHARA NA MARUPURUPU YA VIONGOZI WAO

Idadi kubwa ya Wamorocco wamefanya maandamano kupinga nyongeza ya mishahara na marupurupu kwa viongozi wa serikali wakisema hatua hiyo ni kumdhulumu mwananchi wa kawaida.
Gazeti la al-Quds al-Arabi linalochapishwa mjini London, Uingereza limeandika kuwa, wakazi wa mji mkuu wa Morocco walimiminina katika barabara za mji huo, Rabat usiku wa kuamkia jana na kupiga kambi mbele ya jengo la bunge la nchi hiyo. Maandamano hayo yaliyoitishwa na harakati ya Februari 20 nchini humo, yalikosoa vikali utekelezwaji wa muswada wa nyongeza ya mishahara na marupurupu ya viongozi wa serikali wakiwamo wabunge na mawaziri. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, waandamanaji walitaka kufutwa nyongeza hizo na badala yake wazingatie matatizo ya wananchi. Aidha maandamano hayo yalihudhuriwa na viongozi wa asasi na makundi kadhaa ya haki za binaadamu nchini Morocco. Inafaa kuashiria kuwa, wabunge na mawaziri nchini humo hujichukulia posho na marupurupu kila pale wanapomaliza vikao, kiasi cha kuwafanya hata baadhi ya viongozi hao kuzitaja posho hizo kuwa sio haki yao.

0 comments:

Chapisha Maoni